KUMBUKUMBU YA WAFAT WA BI FATMA (A): KHUTUBA YA BIBI FATIMAH JUU YA FADAK

 KUMBUKUMBU YA WAFAT WA BI FATMA (A): KHUTUBA YA BIBI FATIMAH JUU YA FADAK

BISMILLAHI R-RAHMANI R-RAHIM

Kila himidi njema anastahiki Allah kwa neema na baraka Zake kubwa, na kila shukurani ziende Kwake kwa kutupa ilham, msukumo na kutufungulia milango ya kheri, na kila sifa njema ni za Kwake kwa yale aliyoyatoa, kuanzia zile neemazote za jumla zinazotuzunguka mpaka zile neema anazotujaalia nazo ambazo daima zinaendelea kutukunjukia na kwa ukarimu Wake mwingi ambao anaendelea kututunukia. Kiwango cha ukubwa wake (hayo anayotutunukia) ni kikubwa mno kiasi kwamba ni vigumu kuhisabika, ujazo wake hauwezi kupimika kwa kipimo chochote na mipaka ya neema hizi iko nje ya ufahamu wa binadamu. Amewalingania (amewataka) watu waonyeshe shukrani zao ili neema hizi alizowajaalia ziendelee kuongezeka na zidumu, amewataka watu wamhimidi na kumsifia Yeye ili neema hizi ziweze kuzidi na akafuatilisha hilo kwa kuwaamrisha wamoumbe zaidi mfano wa hayo (huko akhera).

Nashuhudia kwamba hapana mungu isipokuwa Allah, pekee, Hana mshirika – kauli ambayo maana yake ya ndani imeelezewa kuwa ni ikhlasi (utakasifu wa nia kwa ajili ya Allah), kauli ambayo njia zake zimepandikizwa sawasawa katika nyoyo na maana yake inaangaza katika akili (fikra). (Allah) Hawezi kudirikiwa na macho, hawezi kuelezewa kwa maneno wala taswira yake haiwezi kuwazwa (kufikiriwa) katika mawazo ya mwenye kuwaza. Asili ya kila alichokiumba hakitokani na kitu chochote kilichokuwepo kabla ya kitu hicho, na alikiumba kila kitu bila kufuata mfano wa kitu chochote kilichokuwepo hapo kabla. Amekipa kila kitu umbo lake kwa nguvu Zake na amekitengeneza chote kwa matakwa Yake bila ya kuwa na haja yoyote ya kukifanya kitu hicho kiwepo au kupata manufaa yoyote ambayo yangeweza kupatikana kwa kukiunda kitu hicho; (ameumba alivyoviumba) ni kwa kuthibitisha tu hikima Yake, kutangaza utiifu Wake, kudhihirisha nguvu na uwezo Wake, kuonyesha udhalili wa waja wake na kunyanyua wito (ulinganio) Wake. Kisha akaweka malipo mema katika utiifu (Kwake) na adhabu katika uasi Kwake, ili kuwafanya waja Wake wajiepushe na kujiweka mbali na adhabu Yake na kuwapa msukumo na tamaa ya kuelekea katika Pepo Yake. Nashuhudia kwamba baba yangu, Muhammad, ni mja Wake na Mjumbe Wake. Alimteua (mtukufu huyo) hata kabla ya kumtuma [kwa kumpa ujumbe], alimpa jina kabla ya kumchagua [kwa ajili ya Utume] na alimteua kabla ya kumtangaza rasmi [kama Mjumbe] – katika wakati ambao viumbe (wengine) walikuwa wamefichika kusikojulikana, wakifunikwa na pazia la kukosekana kwa uhakika (uyakini) (wa uwepo wao) na huku wakiwa karibu zaidi na ncha ya kutokuwepo kwao – (yote haya ni) kutokana na elimu ya Allah, Aliye Juu, kuhusu khatma ya matokeo ya kila jambo, utambuzi (Wake) kamili wa matukio ambayo yatabainika na kujulikana na utambuzi (Wake) wa hakika na usio na shaka wa hatima ya mambo yote. Allah alimtuma yeye ili kukamilisha misheni Yake (aliyoianza tangu kwa mtume wa kwanza), kusimamisha nidhamu Yake na kutekeleza rehma Zake. [Mtume huyo (S)] Aliwakuta watu wakiwa wamegawanyika katika imani zao, huku baadhi wakiwa ni wenye kuizunguka na kuiabudu myoto (uwingi wa moto) yao, wengine wakiabudu masanamu yao na kumkanusha Allah, licha ya kuwa na utambuzi wa ndani kumuhusu Yeye. Kwa hiyo, kupitia baba yangu Muhammad (S), Allah aliwapa mwangaza katika kiza chao, aliondosha ukinzani kutoka katika nyoyo zao na akatia nuru kiza kilichokuwa katika macho yao. Alisimama miongoni mwa watu akiwa na muongozo, akawaokoa kutokana na upotevu, aliwaondolea upofu wao (wa kiroho), akawaongoza kuelekea kwenye imani sahihi na akawalingania kuelekea kwenye njia iliyonyooka. Kisha Allah akamchukua kurejea Kwake kwa mchukuo wa kiupole, wa kipekee, kiraghba na kiupendeleo.

Kwa hivyo Muhammad (S) hivi sasa yupo katika raha na faraja, [akiwa yuko huru] kutokana na tabu za dunia hii, akizungukwa na malaika watakatifu na katika radhi za Mola Msamehevu, akiwa sambamba na Mfalme Mwenye nguvu. Allah azidishe rehma na amani kwa baba yangu, Mtume Wake, Mlinzi wa wahyi Wake, mja Wake mteule, ambaye alimteua kutoka miongoni mwa viumbe Wake na ambaye ni mwenye kumridhia zaidi. Amani, baraka na rehma za Allah ziwe juu yake.

Kisha Bibi Fatima (s.a.) aliwageukia watu waiokuwepo katika mkusanyiko huo na kusema: Nyinyi ni waja wa Allah, walengwa (wapokezi) wa maamrisho Yake na makatazo Yake, mliobeba dini Yake na wahyi Wake na ni waamana wa Allah juu ya nafsi zenu. Nyinyi ni wafikishaji wa ujumbe Wake kwa watu wote. Ukumbusho wa kweli upo miongoni mwenu, ikiwa ni turathi ambayo yeye (Mtume) amewarithisha na kuiacha pamoja nanyi, akiipa mamlaka juu yenu – (ambacho ni) Kitabu cha Allah chenye kutamka, Quran ya Kweli, Nuru yenye kumulika, mwanga wenye kuangaza – kikiwa na hujja zake zenye kubainisha, na siri zake zilizo wazi. Ujumbe wake wa dhahiri uko wazi na wale wenye kuufuata huwa sababu ya kuonewa wivu. Wenye kushikamana nao wanaongozwa kwenye radhi za Allah na wenye kuuzingatia wananusurika. Kupitia ujumbe huu (wa Quran) hoja za Allah zenye kutoa mwangaza, hukumu Zake za wazi, makatazo Yake yaliyohadharishwa, kauli Zake zisizo na utata, ushahidi Wake wa kutosha, matendo Yake yaliyofadhilishwa, huruma na upole Wake, na sheria Zake zilizoandikwa hupatikana ndani yake.

 Allah aliijaalia imani (Iman) kuwa ni njia ya kuwatakasa dhidi ya ushirikina (shirk), (aliijaalia) swala (Salat) kama njia ya kuwaweka huru na kibri na jeuri, zaka (Zakat) kama njia ya kusafisha nafsi na kuongeza rizki, swaumu (Siyam) kama njia ya kujenga na kuimarisha ikhlasi (nia safi kwa ajili ya Allah), hija (Hajj) kama njia ya kuinua utajo wa dini, uadilifu kama njia ya kudumisha na kuendeleza muunganiko na utulivu wa nyoyo, (amejaalia) utiifu kwetu sisi (Ahlal-Bayt) kama njia ya kudumisha na kuendeleza nidhamu ndani ya umma, uongozi wetu (Imamah) kama njia ya kujilinda kutokana na kugawanyika, jihadi tukufu (Jihad) kama ni utukufu na hishima ya Uislamu, amejaalia subira kama msaada katika kumfanya mtu astahili kupata malipo mema, amejaalia kuamrisha mema (amr bil-maʿruf) kama ni njia ya kuleta islahi na kuurekebisha umma, amejaalia hishima kwa wazazi kama njia ya kujilinda na ghadhabu (za Allah), kuunga undugu katika familia kama njia ya kuongeza idadi yenu, amejaalia kisasi (Qisas) kama njia ya kuzuia umwagaji wa damu, kutekeleza ahadi kama njia ya kupata msamaha, uaminifu katika vipimo na mizani kama njia ya kuepuka upunguaji (katika rizki, mazao, mali,n.k.), kukataza unywaji pombe kama njia ya kujiweka huru na uchafu, kujiepusha na kashfa (kukashifu) (umbea, usengenyi) kama njia ya kujikinga na laana na kujiepusha na wizi kama njia ya kudumisha na kuendeleza tabia njema (Iffah). Alikataza ushirikina ili kuufanya Ulezi (Rubuubiyya) Wake uwe ni wa kipekee,

 “basi mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.” (3:102)

 Mtiini Allah katika yale aliyoyaamrisha na aliyoyakataza kwani kwa hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale wenye ujuzi.’” (35:28)

 Kisha akaendelea:

Enyi watu, tambueni kwamba mimi ni Fatimah na baba yangu ni Muhammad (S). Nawaambia tena, na nnachosema si uongo na nnachokifanya si katika kuchupa mipaka.

“Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe;

yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa

Waumini ni mpole na mwenye huruma.” (9:128)

Kwa hiyo kama mnamtukuza na kumjua yeye, basi mtatambua kwamba yeye ni baba yangu na si baba wa yoyote miongoni mwa wanawake wenu. Yeye ni kaka wa binamu yangu [na mume wangu], na si (kaka) wa yoyote katika wanaume wenu. Ni ubora ulioje kuwa na mahusiano naye. Alifikisha ujumbe, aliwaonya watu wazi wazi, alifanya kazi kubwa dhidi ya njia na mienendo ya washirikina, akivunja migongo yao na kukaba makoo yao. Aliwalingania katika njia ya Mola wake “kwa hikima na mawaidha mazuri.” (16:125)

Alivunja masanamu na kuviponda vichwa (vya uasi) wa washirikina mpaka waliposhindwa na kuangamizwa na kulazimishwa kukimbia. Kisha kiza cha usiku kikaondoka na mpambazuko wa alfajiri ukajitokeza na ukweli ukadhihiri katika sura yake halisi na ya kweli.

Wakati kiongozi wa dini (Mtume) alipozungumza, mapovu yalifoka kutoka kwenye midomo ya washirikina na wakanyamazishwa; kundi dhalili la wanafiki liliangamia na ushirika kati ya kufru na chuki ukavunjika.

Nyote nyinyi mlitamka maneno ya ikhlasi (Tawhidi) na mlikuwa miongoni mwa kundi la watu wenye sura zenye kung’aa na wenye matumbo yenye njaa (wenye kufunga) na kwa hakika “mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto…” (3:103). Nyinyi mlikuwa ni shabaha (maji) ya mnywaji mwenye kiu na mlikuwa ni chombo katika mikono walafi wenye matamanio. Nyinyi mlikuwa ni moto wenye kuwakawaka na ni mahala pa makanyagio ya watu wengine. Mlikuwa mkinywa maji machafu kutoka kwenye mifereji iliyopo kando kando ya njia, na mlikuwa mkila ngozi chafu zilizokaushwa za wanyama au majani. Mlikuwa ni watu dhalili msio na hadhi yoyote miongoni mwa watu mkihofia kutekwa na watu wanaowazunguka.

Kisha Allah, Tabaaraka Wa Taala, akawaokoa kupitia Muhammad (S), baada ya majanga yote haya na baada ya kuteseka katika mikono ya watu washenzi, (ambao ni) Waarabu walio mithili ya mbwa mwitu, na Watu wa Kitabu ambao ni waasi na wapinzani.

 “Kila mara wanapo washa moto wa vita, Mwenyezi Mungu anauzima.” (5:64)

Wakati wowote pembe ya (wafuasi wa) Shetani walipojidhihirisha au wakati wowote watu washenzi miongoni mwa Waarabu walipofungua midomo yao ya wivu na husuda, Mtume (S) alikuwa akimpeleka ndugu yake (Imam Ali) kwao. Ndugu yake huyo (a) alikuwa akiwasambaratisha na kuzima moto wao kwa upanga wake.

Alifanya bidii kubwa kwa ajili ya Allah na alifanya juhudi kubwa katika njia ya Allah. Alikuwa karibu mno na Mtume wa Allah (S), alikuwa ndiye kiongozi (bwana) miongoni mwa mawalii wa Allah, daima alikuwa ni mtu aliyejiandaa, mtayarifu, mchangamfu, mkakamavu, mwenye nia safi na ya dhati, mpole na mchapa kazi – bila kuwa na khofu kamwe juu ya lawama ya yoyote mwenye kulaumu. Wakati huo huo nyinyi mlikuwa mkiishi maisha ya raha na starehe; mkiwa mmetulia bila kusumbuliwa na chochote na mkifurahia kuwa katika raha na usalama. Kisha mkangojea kwamba sisi, Ahlul Bayt, tuzingirwe na hali ngumu na mambo kutugeukia, mkisubiri kwa hamu kubwa kusikia khabari [ya kushindwa kwetu], huku mkikimbia kutoka kwenye uwanja wa vita na kurudi nyuma kwenye mapambano!

Hivyo, wakati Allah alipochagua kumchukua Mtume Wake kutoka kwenye dunia hii ya mapito na kumpeleka kwenye makaazi ya mitume Wake na waja wake wateule, hapo ndipo miba za unafiki zilipodhihirika miongoni mwenu na vazi la dini lilipopasuka. Wale waliopotoka, ambao hapo awali walikuwa kimya, wakaanza kuzungumza, wachache wasiojulikana wakaibuka, na waongo wakajitokeza mbele, wakitoa milio mithili ya punda, wakitembea kwa mikogo, wakitikisa mikia yao katika vikao vyenu na hadhara zenu. Shetani aliinua kichwa chake kutoka katika maficho yake na kuwalingania (kuwaita kwake). Akawapata nyinyi ni wenye kuitikia wito wake na wenye kujali hila zake na udanganyifu wake. Kisha akawashawishi na kuwalaghai na akawakuta kuwa ni wepesi wa kushawishika na kuamshwa; akawaghadhibisha na akawapata kuwa ni wepesi wa kughadhibika. Kwa hiyo mkawatia alama (muhuri) ngamia ambao hawakuwa mali yenu (yaani mkapora haki za wengine) na mkaingia katika manywesheo ambayo si yenu. Na mliyafanya yote haya katika kipindi ambacho haukuwa umepita muda mrefu tangu kuondoka kwa Mtume na kidonda (cha kifo chake) bado kilikuwa kimechimbika na nyoyo zetu zilikuwa bado hazijapona, na hata mwili wa Mtume ulikuwa bado hata kuzikwa katika kaburi! Mlifanya haraka mkidai kwamba mlikuwa mkichelea uasi (mfarakano); “Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina. Na hakika Jahannamu imewazunguka makafiri.” (Q9:49)

Yawe mbali hayo na nyinyi! Vipi nyinyi mna nini? Na wapi mnaelekea wakati Kitabu cha Allah kipo miongoni mwenu? Ambacho mambo yake yapo Dhahiri na hukumu zake ni zenye kuangaza (zenye nuru), alama zake ni zenye kung’aa, makatazo yake ni ya dhahiri na amri zake ni za wazi. Lakini bado mmekitupa (Kitabu hicho) nyuma ya migongo yenu. Je mnataka kuachana nacho kwa sababu ya chuki? Au mnataka kuhukumu (kuendesha mambo) kwa (kitabu) kingine?

“Ni ovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu!” (18:50)

 “Na anaye tafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri (kupata khasara.” (3:85)

 Kisha hamkusubiri hata tufani (Dhoruba) kutulia! Badala yake mkafanya haraka kuchukua khatamu (za ukhalifa) katika mikono yenu. Baada ya kuupata (huo ukhalifa), mkaanza kuwasha upya moto wa uasi na mkashughulishwa katika kuzidi kuuchochea moto huo. Muliitikia wito wa Shetani mwenye kushawishi na mkadhamiria kuzima nuru ya dini yenye kung’aa na kuzuia mafundisho ya Mtume Mtukufu, kisha mkafurahia kula ‘mapochopocho’ ya ukhalifa na kuwapinga Ahlul Bayt kwa siri na kwa dhahiri.

 Hatuna khiyari isipokuwa ni kuvumilia kukatwa kwa makali ya majambia yenu na kupasuliwa miili yetu kwa ncha za mikuki yenu.

 Na hivi sasa (kama haitoshi) mnadai kwamba hatuna urithi wowote kutoka kwa Mtume wa Allah!

 “Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya? Na nani aliye mwema zaidi katika

kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini?” (5:50)

Hivi nyinyi hamtambui? Bila shaka iko wazi mithili ya mchana wa jua lenye kuwaka kwamba mimi ni binti wa Mtume wa Allah!

 Enyi Waislamu, je ni sawasawa kwa mimi kunyimwa mirathi yangu?!

Ewe mwana wa Abu Quhafah (Abu Bakr)! Je, imeandikwa ndani ya Kitabu cha Allah kwamba wewe unaweza kurithi kutoka kwa baba yako lakini mimi siwezi kurithi kutoka kwa baba yangu?

 “Hakika umeleta kitu cha ajabu!” (19:27)

 Je, mmekiacha kwa makusudi Kitabu cha Allah na kukitupa nyuma ya migongo yenu? Wakati (Kitabu hicho) kinasema: “Na Sulaiman alimrithi Daudi” (27:16)

 Na wakati ikisimulia khabari ya Yahya ibn Zakariyya, wakati (Zakariyya)

aliposema: Basi nipe mrithi kutoka kwako. Atakaye nirithi mimi na awarithi ukoo waYaaqub (19:5-6)

 Na inaendelea kutamka:

 Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi

(kurithiana wao kwa wao) katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu.” (8:75)

 Na:

 “Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili” (4:11)

 Na:

 kama akiacha mali — afanye wasia kwa wazazi wake na jamaa zake kwa namna nzuri inayo pendeza. Ni waajibu haya kwa wachamngu.” (2:180)

 Lakini bado unadai kwamba sina haki ya kurithi na siwezi kurithi chochotekutoka kwa baba yangu?!

 Je, Allah ameteremsha aya makhsusi [ya Qurʾan] kwenu nyinyi ambayo alimtoa baba yangu kutoka katika aya hiyo (hakumuhusisha)? Au mnasema kwamba watu wenye imani (dini) mbili tofauti hawawezi kurithiana wao kwa wao? Je, si kweli kwamba baba yangu na mimi tupo katika imani moja? Au nyinyi mna elimu kubwa zaidi juu ya hukumu makhususi na za jumla za Qurʾan kuliko baba yangu na binamu yangu (Imam Ali)? Basi shikeni hatamu zake (ichukueni hiyo Fadak) mpaka tutakapokutana nanyi Siku ya Hukumu; na Allah Ndiye atakayekuwa Hakimu bora na Muhammad ndiye atakayekuwa mlalamikaji katika siku hiyo, na muda wetu wa kukutana ni siku ya Ufufuo siku iliyoahidiwa ambapo waongo (watu wa batili) watakuwa ndani ya khasara kubwa na majuto yao (katika siku hiyo) hayatakuwa na manufaa yoyote kwao!

 “Kila khabari ina kipindi chake” (6:67)

 “Nanyi hivi karibuni mtakuja jua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu.” (11:39)

Kisha akiwakhutubia Ansar, alisema:

Enyi kundi la watu majasiri wenye ufahamu, wenye kuunga mkono (wasaidizi wa) imani na wenye kuuhami na kuutetea Uislamu, ni kipi kilichowasibu mpaka mkaghafilika katika kutetea haki zangu na huku mkishuhudia dhulma zikifanywa dhidi yangu? Je, baba yangu, Mtume wa Allah (S), hakusema: “Mtu anahishimiwa (anatukuzwa) kupitia kizazi chake”? Ni haraka mno mmebadilika na mmetusaliti kwa haraka sana huku mkiwa na uwezo wa kunisaidia na nguvu za kunisapoti katika kile nnachokitaka na kukitafuta.

 Je, mnasema Muhammad (S) amekufa na hakuna jukumu juu yetu”? kwa hakika kumpoteza yeye ni jambo kubwa ambalo khasara yake ni pana, na ufa uliojitokeza (katika Uislamu) ni mkubwa mno na migawanyiko ni mikubwa. Umoja umevunjika na kusambaratika, Dunia imezingirwa katika kiza kizito kutokana na kutokuwepo kwake (Mtume), jua na mwezi vimepatwa, na nyota zimetawanyika! Matumaini yamekatika, milimba imeporomoka na kusambaratika, familia ya Mtume imepotea na utakatifu wao umevunjwa baada ya kifo chake (Mtume)! Wallahi huu ni msiba mkubwa mno na ni maafa makubwa, hakuna balaa kubwa linalowezwa kuinganishwa na balaa hili na hakuna msiba mkubwa zaidi kuliko kifo cha Mtume.

 Jambo hili (kifo cha Mtume) tayari limefikishwa kwenu katika Kitabu cha Allah (swt). Mlikuwa mnasoma Qur’an mchana na usiku kwa sauti kubwa, mkisikitika, katika sauti ya kawaida na katika sauti nzuri. Amma kuhusu yaliyotokea huko nyuma kwa Mitume na Manabii wa Allah kutoweza kukwepa kanuni isiyo na shaka ya kifo na hukumu isiyoepukika ya mauti, Quran inasema:

 “Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakaye geuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao mshukuru.” (3:144)

 Enyi Wana wa Qaylah! Je, nnaporwa urithi wa baba yangu huku nyinyi

mkiangalia na kunisikia? Na huku mkiwa mmekaa na kukusanyika hapa? Mnajihusisha na madai (ya jambo fulani) na mnatambua (ukweli wa) jambo hilo, nanyi mko wengi kwa idadi na mna zana za kutosha, mnamiliki nyenzo na nguvu, na mnamiliki sialaha na ngao za kivita. Kadhiya imewafikia, lakini mmekaa kimya bila ya kuwa na mwitikio wowote juu ya kadhiya hiyo. Mnasikia kilio (changu) lakini hamnisaidii ingawa manjulikana kwa ujasiri na ushujaa wenu na mnasifika kwa kuwa ni watu wazuri na wema; nyinyi ni kundi la watu wateule na walio bora kabisa miongoni mwa wale walioteuliwa. Mlipigana na (Waarabu) wapagani na mkavumilia shida na maumivu. Mlikabiliana na mataifa na mkapambana na mabingwa. Sisi hatujasimama (hatujaacha kufanya hayo), au ni nyinyi, ndio ambao mmesimama? Daima mlifuata amri; tuliamrisha nanyi mkatii. Mpaka pale, kupitia sisi, Uislamu ukasimamishwa na maziwa ya mafanikio yakaanza kumiminika na kutiririka, ushirikina ukashindwa, furaha ya batili kuzimwa, myoto (uwingi wa moto) ya ukafiri kuzimwa, wito wa uasi kunyamazishwa na nidhamu ya dini ikaasisiwa.

 Basi vipi mmejiingiza katika mkanganyiko baada ya ubainifu? Kwa nini

mmekuwa wasiri baada ya kuwa wawazi? Kwa nini mmerudi nyuma baada ya kuwa kwenye mstari wa mbele? Na kwa nini mmekhiyari ushirikina baada ya imani [ya kumuamini Allah]?

“Je, hamtapigana na watu walio vunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumfukuza Mtume, nao ndio walio kuanzeni mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumwogope, ikiwa nyinyi ni Waumini.” (9:13)

 Ah! Tazama! Nawaona mmeelemea maisha ya raha na starehe, na kujiweka mbali na yule ambaye ana haki zaidi katika kutoa au kuzuia (kwa ajili yake). Mmejitenga (na kujiweka) kwenye maisha ya starehe na mmeepuka shida na tabu kwa kukimbilia kwenye raha na utajiri. Kwa hivyo mmekitema kile mlichokuwa mmekizuia (mlichokuwa mmebaki nacho) na mmekitapika kile mlichokuwa mmekimeza.

 “Na Mkikufuru nyinyi na wote waliomo duniani, hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa.” (14:8)

 Nimeyasema yale niliyopaswa kuyasema huku nikitambua fika dhamira (nia) yenu ya kunitelekeza (kutonisaidia) na usaliti wenu uliofyatuka na kuchipua katika nyoyo zenu. Lakini malalamiko yote haya ni natija (matokeo) ya huzuni ya moyo (wangu) na ghadhabu ya ndani (ambayo nnaihisi) na (najua kwamba) haina manufaa yoyote, lakini nimeyasema haya ili kudhihirisha huzuni yangu ya ndani na kutimiza hoja yangu juu yenu.

 Kwa hiyo shikeni khatamu zake (hiyo Fadak, akiifananisha na kipando cha mnyama kama vile farasi au ngamia) na fungeni kisawasawa tandiko lake, kwani ni dhaifu na mnyonge, huku daima aibu yake na fedheha yake itabaki juu yenu. Alama ya ghadhabu za Allah Mwenye nguvu (Jabbar) imewekwa juu yenu, itakuwa ni fedheha ya kudumu kwenu na itawapeleka katika “Moto wa Mwenyezi Mungu uliowashwa. Ambao unapanda nyoyoni.” (104:6-7),

 Kwani chochote mnachokifanya kinashuhudiwa na Allah, “Na wanaodhulum watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.” (26:227)

Mimi ni binti wa “Mwonyaji kwenu kabla ya kufika adhabu kali” (34:46)

“Fanyeni muwezavyo, nasi pia tunafanya. Na ngojeni, na sisi tunangoja.” (11:122)

Baada ya kuyasema haya, Abu Bakr akasema:

Ewe binti wa Mjumbe wa Allah! Bila shaka na kwa hakika baba yako alikuwa mwema, mkarimu, mpole na mwenye huruma mno kwa Waumini, na makafiri watakabiliwa na adhabu yenye kuumiza na mateso makubwa. Tukiangalia mahusiano yake, tunakuta kwamba yeye alikuwa baba yako ghairi ya wanawake wengine, na kaka wa mume wako ghairi ya maswahaba (wake) wengine wote wa karibu. Alimfadhilisha zaidi yeye juu ya kila rafiki na yeye, kwa upande wake, alimsaidia katika kila jambo muhimu. Hakuna anayekupendeni nyinyi isipokuwa ni mtu mwenye saada (furaha) na hakuna anayekubughudhini (anayekuchukieni) isipokuwa ni mtu mwovu. Nyinyi ni kizazi kitakatifu cha Mjumbe wa Allah, wabora wa wateule wa Allah, nyinyi ni wenye kutuongoza katika kheri na (nyinyi) ni njia yetu ya kuelekea Peponi. Na wewe, Ewe mbora wa wanawake wote na binti wa mbora wa Mitume, ni mkweli katika maneno yako na wa kwanza kabisa katika uwezo na kipawa cha akili yako. Hautapokonywa haki yako na wala ukweli wako hautopingwa.

 Wallah (naapa kwa Mungu), kamwe sijapinga maoni ya Mjumbi wa Allah, na kamwe sijafnya kitu chochote isipokuwa kwa idhini yake. Payonia (askari aliye mstari wa mbele) hasemi uongo kwa watu wake; namfanya Allah kama shahidi yangu, na Yeye anatosha kuwa ni shahidi, kwamba nilimsikia Mjumbe wa Allah (S) akisema: “Sisi, kundi la Mitume, hatuachi urithi si wa dhahabu wala fedha, si nyumba wala ardhi; sisi tunaacha tu urithi wa Kitabu, hikima, elimu na utume, na chochote tunachokimiliki katika mali (yenye kuzalisha mapato), (basi hicho) ni kwa ajili ya mtawala anayekuja baada yetu kukigawa kwa namna anavyoona yeye (kwa mujibu wa hukumu yake).” Na tayari tumetumia kile unachokiomba, kwa ajili ya kujipatia farasi na silaha ambazo Waislamu wanaweza kuzitumia katika vita, kupigana dhidi ya makafiri na kuzima uasi wa waasi. Hili lilifanyika kwa makubaliano ya Waislamu wote; sikufanya uamuzi huu peke yangu na kamwe sikulazimisha maoni yangu kwa yoyote.

 Hii hapa ni hali yangu na mali yangu, hiyo ni yako na naiweka mbele yako. Hakuna kitu kitakachozuiwa kwako na hakuna kitu kitakachofichwa kwako. Wewe ni mwanamke mtukufu wa umma wa baba yako na mti mtakatifu kwa ajili ya watoto wako. Hakuna awezaye kupinga fadhila zako, na hakuna awezaye kushusha hadhi ya nasaba yako na asili yako tukufu. Amri yako kuhusiana na kile nnachokimiliki itatekelezwa. Basi je, unaona nnaenda kinyume na baba yako (SAWW) katika jambo hilo?

 Bibi Fatima (s.a.) akajibu:

 Utakasifu ni wa Allah (Subhanallah)! Baba yangu, Mjumbe wa Allah (S), kamwe hakuenda kinyume na Kitabu cha Allah, wala hakupinga hukumu zake. Badala yake ni kwamba, alifuata maelekezo yake na akashikamana na mafundisho yake mema na adhimu. Vipi unapigia chapuo (unaupamba) udanganyifu wako kwa kumuhusisha Mtume na (madai ya) uongo? Na (hila) hii baada ya kifo chake inafanana sana na zile hila zenye madhara zilizopangwa dhidi yake katika kipindi cha uhai wake. Hiki hapa Kitabu cha Allah, ambacho ni hakimu mwadilifu na chenye kutamka kwa ufasaha, (kwa ubainifu wa wazi) kinasema:

 “[Mrithi] Atakaye nirithi mimi na awarithi ukoo wa Yaaqub.” (19:6) Na “Na Sulaiman alimrithi Daudi” (27:16)

 Na Allah Mtukufu akabainisha jinsi gani viwango vya mgawanyo wa mirathi vinatakiwa vifanyike na akaweka sheria za mambo ya wajibu yenye kufungamana na wazazi na watoto na mambo ya mirathi, akaelezea kiwango kinachostahiki kwa wanaume na wanawake, na kwa (kufanya) hivyo basi kuondoa visingizio vya waongo na wapotoshaji na kufuta kabisa wasiwasi na shaka katika akili nan yoyo za wale walioachwa nyuma. Hapana, sivyo hivyo!

 “Bali nafsi zenu zimekushawishini kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayo yaeleza.” (12:18)

 Abu Bakr akajibu:

 Allah alizungumza ukweli na hivyo hivyo Mtume Wake. Na binti yake pia amezungumza ukweli. Kwa hakika bila shaka yoyote wewe ni chimbuko la hikima, maskani ya uongofu (muongozo) na rehma, nguzo ya dini (imani) na chemchem ya hoja. Sikanushi maneno yako sahihi kabisa, na wala sikatai unachokisema. Hawa hapa Waislamu walio mbele yetu ndio walionilazimisha mimi kukubali kile nilichokubali, na ni kwa itifaki yao ya pamoja ndio nikachukua nilichochukua; si kwa nguvu wala ukaidi wala kujipa upekee (kuipa nafsi yangu umuhimu zaidi ya wengine) na wao ni mashahidi wa suala hilo.

Kisha Fatimah (‘a) akawageukia watu na kusema:

Enyi watu wenye kufanya haraka katika kusema maneno ya batili! Enyi wenye kuridhika na matendo mabaya na machafu yatakayoleta maangamizi!

 “Je! Hawaizingatii hii Qur’ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli?” (47:24)

 La hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zenu maovu mliyoyafanya na kwa hivyo usikivu wenu na uoni wenu vimeondoshwa na mmefanya makosa makubwa katika kuifasiri (Qurʾan); mmeirejea Qur’ani kwa njia mbaya mno isiyo sahihi, na ni uovu mkubwa mno wa ufahamu wenu na tafsiri yenu kutoka katika Qur’ani. Wallah, mtaukuta mzigo wake ni mzito na athari zake ni za kutisha, wakati pazia itakapokunjuliwa na balaa kubwa ambalo linafuata litakapokuwa dhahiri kwenu, na kutadhihirika kwenu kutoka kwa Mola wenu yale ambayo kamwe hamkuyahesabu (hamkuyategemea),

 

“na hapo ndipo wale wapotofu (waliosimamia uongo na batili)

watakapokuwa wenye kupata khasara.” (40:78)

 

Mwisho kabisa, aligeukia kaburi la Mtume Mtukufu (saww) na kusoma beti zifuatazo:

Baada ya wewe kufariki, khabari (za uzushi) na machafuko yalifuatia,

Laiti kama ungelikuwepo, basi adhabu na mateso yasingelikithiri kiasi hiki,

Tunakukosa (tunakutamani) kama ardhi kavu inavyotamani mvua,

Na umma wako upo kwenye mkanganyiko, tazama walivyogeuka,

 

Kila familia ina ndugu (jamaa) lakini nafasi (adhimu) mbele ya Mungu, ni kwa wale walio karibu zaidi (na wewe),

Watu wamedhihirisha dhidi yetu kile kilichofichika katika nyoyo zao,

Punde tu ulipoondoka na pazia (kizuizi) la vumbi (udongo) lilipotutenganisha na wewe, walitukunjia uso (walituchukia) na kututukana,

Ulipoondoka, na ardhi yote iliporwa,

Wewe ulikuwa ni mbalamwezi na nuru yenye kuangaza, Kutoka kwa Mungu Mtukufu,

 juu yako Kitabu kiliteremshwa

Jibraʾil alikitufariji kwa aya alizozileta,

Lakini hivi sasa haupo nasi, basi na kheri zote zimetoweka

Ah! Natamani mauti yangelitufika sisi kabla yako__

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *