Sauti ya Bilal | Online Radio

MAADHIMISHO YA MAULID YA MTUME MUHAMMAD (S) 1444 (A.H)-2022 (A.D) – KUSIMAMIA MAADILI N I JUKUMU LETU SOTE.

 MAADHIMISHO YA MAULID YA MTUME MUHAMMAD (S) 1444 (A.H)-2022 (A.D) – KUSIMAMIA MAADILI N I JUKUMU LETU SOTE.

Kwa ujumla tunapozungumzia maadili tunalenga kubainisha tabia au mwenendo wa mtu ambao una picha mbili, moja ni ya ndani na haionekani, na nyingine ni ya nje ambayo mara nyingi ndiyo tafsiri ya picha ya ndani.

Inaposemwa kuwa; “Fulani ana maadili mema, maana yake ni kwamba mtu huyo ni mzuri wa tabia ndani na nje.”

Kwa hali hiyo basi, uzuri wa ndani au ubaya wa ndani ya mtu, huonekana kupitia vitendo vyake, kwa maana vitendo vtendo vikiwa vizuri na vinaungwa mkono na sheria, basi hapo mtu huyu atatajwa kuwa ni mwenye maadili mazuri. Ama vitendo vya mtu vinapokuwa vibaya na haviungwi mkono na sheria, basi mtu huyo hutajwa kuwa maadili yake siyo mazuri au tabia yake siyo nzuri.

Maadili ya Kiislamu

Dini zote kabla ya Uislamu, zilikuja na lengo la kumfanya mwanadamu afikie ukamilifu wa roho na mwili ili awe mwakilishi bora wa Mwenyezi Mungu duniani kwa kuijaza dunia maadili mema na matukufu.

Kwa vile sharia ya Kiislamu imekuja kukamilisha mafundisho ya mbinguni, imejumuisha yale yote yaliyotajwa katika sheria zilizotangulia kuhusu mafundisho ya dini, katika maadili na hukumu za sheria, umeongeza mengi na kurekebisha baadhi yake kulingana na mahitaji ya zama.

Mpaka hapa inatubainikia kuwa, maadili yanayofunzwa na Uislamu, ambayo maana yake ni mwanadamu kujipamba kwa sifa njema, sio tu yanalenga kufundisha namna bora ya kuishi na watu mmoja mmoja au jamii, bali sambamba na hilo, unamtaka mwanadamu kuchunga  maneno na vitendo vyake.

Kwa hali hiyo, maneno na vitendo hivyo ni lazima vizingatie kanuni, na maelekezo yanayohusiana na imani ya Kiislamu na sharia zake, kupitia vyanzo vyake vya msingi ambavyo ni Qur’an na Sunna za Mtume (s) na Maimamu wazawa wa nyumba ya Mtume (a). Kwa mantiki hiyo basi, Uislamu unalitazama suala la maadili kuwa ndiyo kiini cha dini au tuseme ndiyo roho yake.

Tunasema hivyo kwa sababu sharia na kanuni za Uislamu pamoja na maelezo yake yote, yanalenga kumfanya mwanadamu awe mcha Mungu ili aweze kufika kwenye kiwango bora cha maisha yatakayomletea furaha duniani na malipo mazuri kesho akhera. 

Maadili katika maandiko ya KiislamuSharia tukufu ya Kiislamu imehimiza mno kuhusu watu kujipamba kwa maadili mema, kama ambavyo imeeleza  fadhila na malipo mengi anayopewa  yeyote mwenye kushikamana na maadili hayo.

Hapa chini tunaorodhesha baadhi tu ya maandiko kama mfano kwani ni mengi mno na nafasi haitoshi kuyaandika kwa wingi.

 Aya tukufu za Qurán. 

1. Mwenyezi Mungu anasema kumwambia Mtume (s): “Na hakika wewe una tabia tukufu.” Qur 68:04Itoshe tu kusema kuwa; suala la maadili au tabia njema ni sifa inayompa mtu utukufu na heshima, na ndiyo maana Mwenyezi amemsifu Mtume wake wa mwisho Muhammad (s) kwa sifa bora ya kuwa na maadili ya hali ya juu, kiasi kwamba sifa hiyo haikutamkwa kwa Mtume mwingine mfano wake.

2. Aidha katika sura ya 3 aya 159 Mwenyezi Mungu anasema: “Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo…” Qur 3:159

Aya hii tukufu inatubainishia wazi kuwa, siri kubwa ya kukubalika kwa Uislamu katika jamii ya watu wa Makka na kwingineko ilitokana na maadili au tabia njema ya Mtume Muhammad (s).

Ndugu msomaji ni vizuri tueleze kidogo ili ufahamu athari ya tabia njema au maadili mema ya Mtume Muhammad (s).

Mnamo mwaka wa 35 tangu kuzaliwa Mtume (s)  al Kaabah ilijengwa upya kutokana na nyufa zilizokuwa zinatishia uimara wake. Hata hivyo baada ya ujenzi kukamilika, Maquraish walizozana kuhusu nani kati ya koo zao za Kiquraish atakayepata heshima ya kuweka Hajarul Aswad mahala pake.

Jambo hili karibu lisababishe mapigano baina yao, lakini hatimaye walikubaliana kuwa mtu yeyote wa kwanza atakayeingia mahala hapo basi huyo atakuwa ndiye msuluhishi wa mzozo huu. Alhamdulillahi ni Mtume Muhammad (s) ndiye alikuwa wa kwanza kuingia mahala hapo na wote kwa pamoja walipomuona wakasema: “Amekuja mtu mwaminifu na sote tunamkubali na kumridhia.”

Matokeo haya yalikuja kutokana na maadili na tabia njema aliyokuwa nayo Mtume Muhammad (s) kabla ya kuanza kazi ya kuwalingania watu kwenye Uislamu.

 Hadithi kuhusu maadili.

1. Amesema Mtume (s) kwamba: “Kwa hakika nimetumwa ili nije kukamilisha (mafunzo ya) maadili mema.”

2. Katika hadithi nyingine anasema: “Watu bora kati yenu ni wale wenye maadili mema, wapole na wenye huruma. Hawa ni wale watu ambao huwazoea (wenzao) na wao kuzoweleka (kwa wenzao) na huwapandisha kwenye vipando vyao.”

3. Naye imam Ali bin Abi Talib (a) amesema: “Hata kama tusingekuwa na matumaini ya kuingia peponi na wala hatuogopi moto wala kuadhibiwa, basi ingetupasa kuwa na maadili mema, kwani maadili mema ni miongoni mwa mambo yanayoelekeza kwenye njia za mafanikio.”

4. Kwenye hadithi nyingine imam Ali (a) anasema: “Maadili mema huleta ongezeko la riziki na kuwaliwaza marafiki.” 

5. Imam Muhammad al Baqir anasema: “Kwa hakika muumini aliyekamilika katika imani ni yule mwenye maadili mema.” 

6. Naye imam Ja’far as Sadiq (a) anasema: “Ikiwa unataka kuhishimiwa basi, uwe mpole, na ikiwa unataka kudharauliwa uwe na ulimi mkali.” 

Wasifu wa Mtume na wazawa wa nyumba yake

Historia inaeleza kuwa, Mtume Muhammad (s) na watu wa nyumbani mwake walikuwa na sifa tukufu katika maadili mema katika kila jambo, kiasi kwamba walifanikiwa kuziteka nyoyo na akili za watu. Si hivyo tu bali walikuwa ni kiigizo chema kutokana na maadili yao na mwenendo wao wa maisha kwa ujumla.

Hapa chini tutanukuu baadhi ya mifano ya tabia na mienendo yao ambayo ni mafunzo tunayopaswa kujifunza.

  1. Imam Ali (s) anaeleza wasifu wa tabia ya Mtume (s) kwa kusema: “Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa mkarimu mno kuliko watu wote, mwenye kifua kipana kuliko watu wote, mkweli mno kuliko watu wote…na alikuwa mkarimu mno kwa ndugu, na mtu yeyote atakaye keti naye na akamjua basi atampenda.” Imam Ali (a) anakamilisha kutaja wasifu wa Mtume (s) kwa kusema: “Sijapata kuona mfano wake kabla wala baada yake.”

 

  1. Katika hadithi nyingine Imam Ali (a) anasema: “…Kamwe Mtume (s) alikuwa hakatishi mazungumzo ya mtu mpaka huyo mtu atakaponyamaza, na hakuonekana kunyoosha miguu mbele ya mtu aliyeketi naye.

 

  1. Naye Anas bin Malik mtumishi wa Mtume (s) kila mara anapokumbuka maadili na tabia njema za Mtume (s) alikuwa akisema: “Nimemtumikia Mtume (s) kwa miaka ishirinilakini kamwe hakuwahi kunikemea wala kuniambia kwa nini umefanya (jambo fulani)…?”

Hii ni mifano michache sana inayohusu mwenendo na maadili mema ya Mtume Muhammad (s) yalivyokuwa.

Kwa ujumla Mtume wetu (s) alikuwa na mahusiano mazuri na mtu mmoja mmoja, jamii na hata watumishi wa nyumbani mwake kama tulivyomsikia Anas bin Malik (r) akisema.

KIJALIZO: Tukamilishe makala haya kwa kubainisha baadhi ya faida zinazopatikana kutokana na tabia njema au maadili mema.

Faida ya kwanza: Ni muhimu kufahamu kuwa, mtu yeyote mwenye tabia njema wakati wote huishi maisha mazuri tena yenye furaha.

Mwenyezi Mungu anasema: “Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutampa maisha mema; na tutawalipa  ujira wao kwa mema waliyokuwa wakiyatenda.”Qur 16:97

Kinyume cha hivyo ni mtu kuishi katika mfumo wa tabia mbaya au maadili mabaya. Mwenyezi Mungu anasema: “Na atakayepuuza mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa ni kipofu.” Qur 20:124

Faida ya pili: Hapana shaka kwamba, tabia njema huondosha na kuyeyusha chuki na fundo la moyo mfano wa barafu inavyoyeyuka katika kipindi cha joto. Aidha kwa sababu ya maadili mema jamii husalimika kutokana na vurugu na kutokuelewana baina ya watu na badala yake upendo, maelewano na kusaidiana huchukua nafasi hiyo.

Mwenyezi Mungu anasema: “Mema na maovu hayalingani. Ondoa uovu kwa lililo jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako na yeye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu.” Qur 41:33-34

Kama ambavyo maadili mema huwavutia watu na wakamsogelea muhusika wa maadili hayo, basi tabia mbaya na maadili mabaya huwakimbiza watu na kuwaweka mbali na mtu huyo kutokana na maadili na tabia yake mbaya.

Mwenyezi Mungu anasema kumwambia Mtume (s): “…Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia…” Qur 3:159

Amani iwe juu yako ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, amani iwe juu yako ewe Mtume uliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu, kuwa ni rehema kwa walimwengu wote.

 

IMETAYARISHWA NA:

KITENGO CHA TABLIGH – THE BILAL MUSLIM MISSION OF TANZANIA

MAKAO MAKUU, DAR ES SALAAM.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *