KUMBUKUMBU YA MIAKA 20 YA KIFO CHA ALLAMAH RIZVI – KIFO CHA MWANACHUONI NI PENGO LISILOZIBIKA: ALLAMAH RIZVI NYOTA INAYONGÁRA 1927-2002
Huenda tunajiuliza ni kwa nini tunapaswa kuwakumbuka wanachuoni wetu mwaka kwa mwaka baada ya kufariki?
Mtume (s) anasema: “Hatofishwa mwanazuoni yeyote yule isipokuwa patatokeza pengo lisilozibika.”
Katika riwaya nyingine imam Ja’far bin Muhammad as-Sadiq anasema: “Anapokufa mwanazuoni hutokea ufa katika Uislamu ambao hauwezi kuzibwa na kitu chochote mpaka siku ya Qiyama.”
Maana ya hadithi hii ni kwamba, nafasi iliyoachwa na mwanazuoni aliyeondoka haiwezi kupata mbadala hata kama baada yake atakuja mwanazuoni bora zaidi kwa elimu kuliko huyu aliyeondoka, kwani huyu aliyekuja siyo yule aliyeondoka bali ni mwanazuoni mwingine.
Riwaya hii kwa namna moja au nyingine twaweza kusema kuwa inamuhusu al Marhoum al Allamah Sayyid Akhtar Rizvi ambaye licha ya kuwa na elimu, ni mwanazuoni aliyekuwa na hekima, moyo wa kujitolea na kumthamini kila mtu bila kujali jinsia, rangi, utaifa wake wala uwezo wake wa mali.
Al Marhoum Sayyid Akhtar Rizvi (Allah amrehemu), ndiyo mwanazuoni wa kwanza wa Kishia aliyeweza kupenya katika jamii ya wazawa wa Tanganyika (Waafrika) kwa ajili ya kuitangaza nuru ya Ahlul Bayt (a). Aidha ni mwanachuoni wa kwanza kutoka Bara Hindi aliyefanikiwa kuwashawishi ndugu zetu wa Jumuia ya Khoja Shia Ithnaa Ashari kuungana naye katika kazi ya kuwafikishia wazawa wa Tanganyika ujumbe huu wa Ahlulbayt.
Bila shaka alikabiliana na vikwazo vingi katika kazi hii ya kubashiria Ushia katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki, lakini alivumilia na akasubiri.
Sifa kubwa na ya kipekee aliyokuwa nayo al Marhoum Sayyid, ni subira, moyo wa kujitolea, unyenyekevu kwa wenyeji wake na mahusiano mazuri na wanazuoni wa Kisunni mfano al Marhoum sheikh Nurdini as Shadhili, sayyid Abdoulqadir Juneid na wengineo.
Unyenyekevu wake, subira na mahusiano hayo mazuri vilimsaidia sana kuwa karibu na wenyeji wa Tanganyika kiasi cha yeye kufaulu kupata wanafunzi wachache aliyoanza kuwafundisha madhehebu ya Shia Ithnaa Sahari.
Watu muhimu wanaopaswa kukumbukwa katika wenyeji hao wa Tanganyika, ni pamoja na al marhoum sheikh Muhammad Ali Ngongabure ambaye madrasa yake ndogo iliyokuwepo Temeke ilitumiwa na Allamah Rizvi kufundisha Fiqhi na Aqaid kwa mujibu wa madhehebu ya Shia. Madrasa hiyo ilikuwa na wanafunzi wapatao 15-20.
Wakati tunakumbuka kutimia kwa taqriban miaka 20 tangu kifo chake, hatuna budi kuzienzi juhudi alizozianzisha katika kufikisha tabligh ya madhehebu ya Ahlubayt (a) katika nchi yetu na maeneo mengine ya Afrika Mashariki, Afrika magharibi na huko Guyana iliyoko Amerika ya Kusini na kwingineko.
Kila mmoja wetu kwa nafasi aliyonayo ndani ya jamii, atumie vizuri nafasi hiyo kwa kutimiza wajibu wake katika kazi hii ya Tabligh ambayo Allama Rizvi (r) ametuachia tuiendeleze.
xxxxx
Imeandaliwa na:
Idara ya Tabligh – BMMT Makao makuu
Dar es salaam.