KUAMRISHA MEMA NA KUKATAZA MAOVU JUKUMU LA KILA MMOJA

 KUAMRISHA MEMA NA KUKATAZA MAOVU  JUKUMU LA KILA MMOJA

Tumo ndani ya mwezi wa Muharram tunamkumbuka bwana wa mashahidi imam Husein (a) aliyeuawa na watawala wa dola ya Banu Umayya chini ya uongozi wa Yazid bin Muawiya. Zama hizo kwa mujibu wa historia maovu na ufisadi wa kila aina vilishamiri.

Lilikuwa ni jukumu la umma kukemea maovu hayo na ufisadi huo, lakini ni imam Husein (a) na wafuasi wake wachache ndiyo waliosimama kukemea maovu hayo.

Imam alitoka na kauli mbiu yake mashuhuri akasema: “Kwa hakika sikutoka kwa (nia ya) ujeuri, wala kiburi, wala ufisadi au udhalimu, bali nimetoka ili  kwenda kuurekebisha umma wa babu yangu, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s). Nataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kufuata mwenendo wa babu yangu na baba yangu Ali bin Abi Talib (a)…”

Kauli mbiu ya imam (a) ililenga kuweka hai faradhi ya kuamrisha mema na kukataza maovu kama alivyosema  Allah (s.w.t) ndani ya Qur’an kwamba: “Na uwepo kutokana na nyinyi umma unao lingania kheri na unao amrisha mema na unakataza maovu… ” Qur 03:104

Ndugu msomaji wa makala haya! Ni miaka mingi imepita tangu kuliwa kwa imam Husein (a) na wafuasi wake. Pamoja na hali hiyo tunapaswa kuendelea kumkumbuka na kumuunga mkono imam Husein (a) na wafuasi wake ambao waliuliwa katika njia ya kuamrisha mema na kukataza maovu.

Imam Husein (a) na wafuasi wake walitimiza wajibu wao katika hili walipokubali kutoa maisha yao ili kuhakikisha umma unaaamka na kutambua wajibu wake katika suala la kuamrisha mema na kukataza maovu ulimwenguni kote.

MAOVU YAMEJAA KILA KONA

Kwa ujumla ulimwengu umejaa maovu ya kila aina, kuanzia mashariki mpaka magharibi, na kaskazini hadi kusini uovu na ufisadi umetawala.

Ubinadamu umetoweka, na yanayotendeka katika jamii ya ulimwengu huu hayafai hata kusimulia.

Kwa maovu yanayotendeka, imekuwa vigumu na wala siyo rahisi kuwarudisha wanadamu kwenye asili ya maumbile aliyoyaumba Mwenyezi Mungu.

Hivi sasa kuna nguvu kubwa sana inatumika kuimarisha maovu na kuvunja misingi yote ya ubinadamu.

Ndugu msomaji! Makala haya mafupi hayakusudii kutaja ni maovu gani yanayoimarishwa kwa nguvu, na ni mema gani yanayosakamwa kwa lengo la kufutwa na kutoweka ndani ya msamiati wa ubinadamu. Tunatosheka na usemi wa Waswahili waliposema: “Mwenye macho haambiwi tazama…”

Kwa hali ilivyo hivi sasa, hadithi ya Mtume (s) ifuatayo itafafanua ni mahala gani tumefikishwa au tumefika.

Inasimuliwa kuwa, siku moja Mtume (s) aliwaambia Maswahaba:  “Je, mtakuwaje (enyi watu) pale wanawake wenu watakapoharibika, na vijana wenu watakapozama kwenye starehe, nanyi mkawa hamuamrishi mema wala hamukatazi maovu? Masahaba wakamwambia: Je, jambo hilo litawezekana  ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Ndiyo. Kisha aliendelea akasema: Mtakuwa na hali gani (utakapofika wakati) mtaamrisha maovu na mema kuyakataza? Masahaba wakasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Itafikia hali kama hiyo? Mtume (s) akasema: Naam, bali na uovu kuliko hilo! Mtakuwa na hali gani (enyi watu)! Utakapofika wakati jambo jema mataliona kuwa ni ovu, na ovu mataliona kuwa ni jema?

Kwa jinsi ulimwengu ulivyo, mema yanaonekana kuwa ni maovu na maovu ndiyo mema.

Ungana na imam Husein (a) katika kuamrisha mema na kukataza maovu. Anza na nafsi yako, familia yako na kisha jamii inayokuzunguka.

IMEANDALIWA NA

OFISI YA TABLIGH

BMMT HQ – DAR ES SALAAM

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *