JE! ALI BIN ABI TALIB (A) ALIKUWA MWOGA?

 JE! ALI BIN ABI TALIB (A) ALIKUWA MWOGA?

Yeyote ukimwambiwa kuwa kuna dhuluma ilifanyika dhidi ya imam Ali bin Abi Talib (a), na watu wa nyumba ya Mtume (s) itamuwia vigumu sana kukuamini.

Ni vigumu kwa sababu Waislamu wengi kama si wote wanafahamu kuwa haiwezekani kumdhulumu mtu mfano wa Ali bin Abi Talib (a), kutokana na ushujaa wake usiyokuwa na mfano baada Mtume Muhammad (s).

Vita vya Badri ni ushahidi tosha kukuonesha ni vipi alikuwa shujaa. Historia inaeleza kuwa siku hiyo, imam Ali (a) peke yake aliuwa washirikina wasiyopungua 30.

Aidha ukija katika vita vya Uhdi, wanahistoria wa Kiislamu wanataja washirikina zaidi ya 20, waliuliwa na imam Ali bin Abi Talib (a).

Lakini siku ya Khandaq imam Ali (s) ndiye pekee aliyejitokeza kumkabili shujaa wa washirikina wa Makka wakati ule, Amru ibn Abdi Wuddi, kwani kablaya yay eye kujitokeza kumkabili mshirikina huyo, hakuna mtu yeyote aliyejitokeza miongoni mwa maswahaba kuitika wito wa Mtume (s) baada ya kunadi mara tatu nani atatatoka kumkabili Amri?!!!

Kwa nini hakutetea ukhalifa wake?

Naam! Inasemwa kuwa, katika kipindi cha Makhalifa watatu wa mwanzo yaani Abu Bakri, Omar na Uthman (r), Ali (a) hakujitokeza kupigania haki yake ya Ukhalifa, wala hakuonesha ushujaa wake kumtetea Fatimah binti Muhammad (a), wala heshima ya nyumba yake.

Hali  hii inawachanganya watu wengi hasa wanapokuja kumuona baadaye akipambana na maswahaba Talha, Zubeir na mama Aisha binti Abu Bakri (r) katika vita ya Jamal. Kisha akapigana na Muawiyah bin Abi Sufiyan katika vita ya Siffin, mambo ambayo yalijiri baada ya Makhalifa wale watatu wa mwanzo kuondoka.

Watu wanajiuliza je, ukimya ule wa Ali (a) ulitokana na woga au udhaifu? Na wengine wanahoji je, huyo ndiyo yule shujaa aliyesifiwa na Mtume (s) siku ya Khaibar kuwa ni Kar-Raarun na siyo Far-Raarin?

Majibu kwa maswali haya

Watu wanapaswa kufahamu kuwa Ali (a) alikuwa ni mteule wa Allah (s.w.t) kwa ulimi wa Mtume Muhammad (s).

Wanapaswa kufahamu pia kwamba, hatua yoyote ile iliyochukuliwa na Ali (a) ilikuwa kwa hekima au ni kutokana na muongozo au kiigizo kutoka kwa wateule wa Allah (s.w.t).

Kwa mukhtasari twaweza kusema kuwa; ukimya wa imam Ali (a) ulitokana na yeye kufuata mwenendo wa Mitume wa Allah (s.w.t) katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na watu wao.

Lakini itoshe tu kusema kuwa, mushkeli huu na maswali kama haya havijaanza leo bali tangu imam Ali (a) akiwa hai watu walijiuliza wakasema:  “Ana nini Ali (a) mbona hakupambana na Abu Bakri, Umar na Uthman kama alivyopambana na Talha na Zubeir?”

Habari hizi zilipomfikia mtukufu huyu wa daraja baada ya Mtume (s), aliamuru panadiwe ili watu wakusanyike. Baada ya mkusanyiko huu wa watu alisimama na kuwahutubia.

Imam Ali (a) alianza kwa kumuhimidi Allah (s.w.t) na kumswalia Mtume (s) kisha akasema: “Enyi watu! Imenifikia habari kwamba, kuna watu wanasema;  ana nini Ali (a) mbona hakupambana na Abu Bakri, Umar na Uthman kama alivyopambana na Talha na Zubeir?”

Aliendelea akasema: “Fahamuni ya kwamba hakika mimi ninacho kiigizo kwa Manabii saba wa Allah (s.w.t) katika jambo hili.

Wa kwanza wao. Nabii Nouh (a) pale Allah (s.w.t) aliposema akieleza habari za Nabii huyo: “…Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi (ewe Mola) ninusuru!” Qur 54:10. Mkisema kuwa hakushindwa mtakuwa mumekufuru na mumesema uongo. Na kama yeye alishindwa, basi Ali anastahiki zaidi udhuru (na kusamehewa kwa alichokifanya)…

Wa pili. Nabii Ibrahim (a) pale aliposema: “Nami najitenga nanyi na hayo mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu…” Qur 19:48. Basi kama mtasema alijitenga nao bila ya kuchukizwa, mtakuwa mmekufuru, na kama mtasema kuwa aliona jambo lenye kuchukiza kutoka kwa watu hao, basi mimi nina udhuru zaidi.

Wa tatu. Nabii Lout (a) pale aliposema: “…Laiti ningelikuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu! Qur 11: 80. Mkisema alikuwa na nguvu, basi mtakufuru na mtakuwa mumeikanusha Qur’an. Na mkisema hakuwa na nguvu, basi mimi nina udhuru zaidi kuliko yeye.

Wa nne. Nabii Yusuf (a) pale aliposema: “Ee Mola Mlezi wangu! Nastahabu kifungo kuliko haya wanayo niitia…” Qur 12:33. Mkisema aliomba maombi hayo bila ya kuwepo karaha na chukizo, basi kwa hakika mtakufuru na mutakuwa mumeikanusha Qur’an. Na kama mtasema kuwa aliomba hivyo kutokana na yanayomchukiza Allah (s.w.t) na akakhiyari kuingia gerezani, basi mimi nina udhuru zaidi kuliko yeye…

Wa tano. Nabii Musa bin Imran  (a) aliposema: “Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.” Qur 26:21. Kama mtasema kuwa Musa (a) hakuwakimbia kutokana na kuchelea madhara juu ya nafsi yake, kwa hakika mtakufuru. Na kama mtasema kuwa alikimbia kutokana na khofu, basi wasii ana udhuru zaidi kuliko yeye…”

Wa sita. Nabii Haroun (a) anaposema: “Ewe mwana wa mama yangu! Hakika hawa watu wamenidharau, na wakakaribia kuniuwa. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu…” Qur 7:150. Kama mtasema kwamba watu hao hawakumdharau na wakakaribia kumuuwa, pale alipowakataza kumuabudia ndama, basi mtakufuru. Na mkisema kwamba wao walimdharau na walikaribia kumuuwa kutokana na uchache wa watu wa kumsaidia, basi wasii ana udhuru zaidi kuliko yeye…”

Wa saba.  Mtume Muhammad (s) pindi alipokimbilia pangoni. Kama mtasema kwamba yeye alikimbia bila ya kuwepo khofu yoyote ile juu ya nafsi yake kutokana na kuchelea kuuliwa, kwa hakika mtakufuru. Na kama mtasema kuwa walimtisha na akawa hana njia isipokuwa kukimbilia pangoni, basi wasii ana udhuru zaidi kuliko yeye…”

(Baada ya maneno haya), watu wote kwa pamoja wakasema: “Amesema kweli Amirul-Mu’minin.”

Je! Wewe unasemaje?

IMETAYARISHWA NA KITENGO CHA TABLIGH HQ-BILAL MUSLIM MISSION OF TANZANIA KWA, MNASABA WA MAADHIMISHO YA GHADIR KHOUM.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *