Sauti ya Bilal | Online Radio

HIJA YA KUAGA NA TUKIO LA GHADIR KHOUM

 HIJA YA KUAGA NA TUKIO LA GHADIR KHOUM

Ghadir Khoum kijiografia:

Ghadir Khoum ni eneo lenye bonde ambalo maji ya mvua hutuama. Bonde hili lipo baina ya miji mitukufu ya Makka na Madina, na ni njia panda ya kuelekea Madina, Misri, Iraqi na Yemen.

 

Ghadir Khoum na matukio muhimu

Inafaa kuashiria kuwa, Mtume (s) alisimama Ghadir Khoum mara tatu kama ifuatavyo:

1. Wakati anahama kutoka Makkah kwenda Madina.

2. Wakati akienda kwenye hijja yake ya mwisho.

3. Wakati anarejea Madina kutoka kwenye hijja yake ya kuaga.

Hija ya mwisho ya Mtume (s)

Tarehe 24 au 25 mwezi wa Dhul Qa’dah mwaka wa 10 hijiriyyah, Mtume (s) aliondoka Madina kuelekea Makka kwa ajili ya kuhiji hija yake ya mwisho ambayo pia huitwa hija ya kuaga. Katika safari hii aliwalingania Waislamu wote kwenye miji ya Kiislamu kwa mujibu wa ramani ya zama hizo na wakaungana naye. Inakadiriwa kuwa watu laki moja na ishirini walishiriki kwenye hija hii.

Kushuka kwa aya ya Tabligh

Baada ya kumalizika kwa hija iliyohudhuriwa na idadi kubwa ya Waislamu, safari ya Mahujaji kurejea makwao ilianza. Walipofika njia ya panda ambayo ni Ghadir Khoum, Mwenyezi Mungu akamteremshia Mtume aya ya 67 sura ya 5, mashuhuri kama aya ya Tabligh akamwambia: “Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.”

Mtume (s) alisimamisha msafara wake na kuagiza wote waliyokwishapita eneo hilo warudishwe na wale ambao hawajafika wangojewe.” Hiyo ilikuwa ni siku ya Alhamisi tarehe kumi na nane Dhul-Hijjah mwaka wa 10.

Taarifa ya Kuaga

Wanahistoria wa Kiislamu wanaeleza kuwa, siku hiyo ilikuwa ni siku yenye jua kali na joto kali kiasi kwamba Maswahaba walilazimika kuweka nguo chini ya nyayo zao kujikinga na moto wa mchanga wa jangwani.
Baada ya watu kukusanyika hapo Ghadir, palinadiwa kwa ajili ya swala ya adhuhuri na Mtume (s) akaswalisha. Alipomaliza kuswalisha alisimama juu ya mimbari iliyotengenezwa kwa magodoro ya ngamia akawahutubia na wote wakimsikiliza.

Alimhimidi Mwenyezi Mungu na kushuhudia juu ya upweke wake na kwamba yeye ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kisha akasema: “Enyi watu! Hakika mimi karibu nitaitwa nami nitaitika, bila shaka nitaulizwa kama ambavyo nanyi mtaulizwa, basi je, mtasema nini?”

Wote walijibu wakasema: “Tunashuhudia kuwa hakika wewe umefikisha na umetunasihi na umetumikia dini vilivyo na Mwenyezi Mungu akulipe mema.”
Kwa mukhtasari alitoa hotuba ndefu yenye usia, maagizo na maonyo kwa umma wa Kiislamu.

Shikamaneni na Qurán na kizazi changu

Miongoni mwa maagizo ya Mtume wetu (s) siku hiyo, aliusia kushikamana na Qurán na kizazi chake watu wa nyumba yake akasema: “Kwa hakika mimi nitakutangulieni kufika kwenye hawdh, na nyie mtanikuta kwenye hawdh, basi angalieni ni vipi mtanifuata katika vizito viwili? (Kizito) kikubwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu ambacho ncha moja imo mikononi mwa Mwenyezi Mungu na ncha nyingine imo mikononi mwenu, shikamaneni nacho msipotee.

(Kizito) kidogo ni kizazi changu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amenieleza kuwa, viwili hivi havitatengana mpaka vinifikie kwenye hawdh. Nami nimemuomba Mola wangu kwa hilo. Hivyo basi msivitangulie viwili hivi mataangamia, na wala msivipuuze mtaangamia.”

Alipokwisha kusema maneno hayo Mtume (s) aliushika mkono wa imam Ali (a) akaunyanyua juu mpaka weupe wa kwapa zake ukaonekana, kisha akamtambulisha kwa watu wote waliyohudhuria hapo akasema: “Enyi watu! Ni nani mbora wa watu kwa waumini kuliko nafsi zao?” Wakasema: “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndiyo wanaojua zaidi.” Mtume (s) akasema: “Hakika Mwenyezi Mungu ni mtawala wangu na mimi ni mtawala juu ya waumini na mimi ni mbora kwa waumini kuliko nafsi zao. Basi ambaye mimi nilikuwa mtawala wake Ali ni mtawala wake.”

Aliyakariri maneno haya mara tatu kisha akasema: “Ewe Mwenyezi Mungu! Mtawalishe atakayemtawalisha, na umfanye adui atakayemfanyia uadui, na umpende atakayempenda, na umchukie atakayemchukia, na umsaidie atakayemsaidia, na umpuuze atakayempuuza na uielekze haki iwe pamoja naye popote alipo.” Kisha Mtume (s) akasema: “Naagiza! Kila aliyeshuhudia haya na amfikishie asiyekuwepo.”

Dini imekamilika

Kabla watu hawajatawanyika na kila mmoja kuendelea na safari yake, ulishuka wahyi wa Mwenyezi Mungu akasema: “Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekuridhieni UISLAMU uwe ndiyo Dini…” Qur 05:03

Mtume Muhammad (s) awaamuru Waislamu kumpongeza Ali (a)

Kilichofuata baada ya kushuka kwa aya tuliyoitaja hapo juu, Mtume (s) aliingia kwenye hema lake akakaa na akamwamuru Ali (a) aketi kwenye hema hilo mkabala naye, kisha akawaamrisha Waislamu waingie humo na wampongeze imam Ali (a) kwa kupata wadhifa huo na pia wamsalimu kwa salamu ya uongozi ambayo ni as-Salamu alaika yaa amiral moominina.

Watu wakafanya kama walivyoamrishwa na Mtume (a) na miongoni mwa waliompongeza mwanzoni kabisa ni Maswahaba Abu Bakr na Umar Ibn Al-Khattab, na kila mmoja wao akisema: “Hongera ewe mwana wa Abu Talib! Leo umekuwa mtawala wangu na mtawala wa kila Muumini mwanamume na mwanamke. Kisha hivyo hivyo Mtume (s) akawaamuru wakeze na wake wa Waumini waliyokuwa pamoja naye katika safari hiyo nao wakafanya hivyo hivyo.

Wapokezi wa Hadithi ya Ghadir

Maswahaba wa Mtume (s) wapatao 100 ni miongoni mwa watu waliyopokea na kusimulia hadithi hii. Tunataja baadhi yao kama ifuatavyo:

1. Omar bin Al-Khattab (r)
2. Othman bin Affan (r)
3. Aisha binti wa Abu Bakr(r)
4. Salman al-Farsi(r)
5. Abu Dhar al-Ghafari (r)
6. Zubayr bin Al-Awwam (r)
7. Jaber bin Abdullah Al-Ansari (r)
8. Abbas bin Abdul-Muttalib (r)
9. Abu Hurayrah na wengineo…

Wapokezi wote hawa walikuwepo siku ya tukio la Ghadiir na walishiriki katika Hijja ya kuaga.

Aya za Qurán zilizoteremshwa siku ya Ghadir.

Wafasiri wa Qurán wapatao 64 wameeleza kuwa kuna aya za Qurán ambazo ziliteremshwa siku ya tukio la Ghadir na wakazitaja kama ifufuatavyo:

1. Aya inayoeleza kukamilika kwa dini kwa mujibu wa mnasaba Mtume (s) kumtangaza imam Ali (a) kuwa ndiye kiongozi baada yake. Hii ni aya ya 3 katika sura ya tano ambapo Mwenyezi Mungu anasema: “Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini…”

2. Aya ya tabligh (kufikisha) ambayo ni ya 67 katika sura ya 5, pale Mwenyezi Mungu anaposema: “Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.”

3. Aya ya 1-3 sura ya 70, pale Mwenyezi Mungu aliposema: “Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea, Kwa makafiri – ambayo hapana awezaye kuizuia -Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja.”

Imethibiti katika vitabu vya tafsiri na Hadith vya wanachuoni wa kutegemewa wa Kisunni kwamba, Mtume (s) alipofika Ghadir Khoum na kufikisha hicho alichokifikisha na habari hizo zikaenea katika miji ya Kiislamu, Numan bin Harith Al-Fihri alikuja kwa Mtume (s) akasema: “Ewe Muhammad, ulituamrisha kwa amri ya Mwenyezi Mungu tushuhudie kwamba hapana Mola ila Mwenyezi Mungu, na kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na (ukatuamuru) tuswali, tufunge swaumu, tuhiji na tutoe zaka, tukakukubalia. Kisha hukutosheka na hayo mpaka ukaunyanyua mkono wa mtoto wa ami yako ukamfadhilisha juu yetu ukasema: yeyote ambaye mimi nilikuwa mtawala wake, basi Ali ni mtawala wake. Je, jambo hili linatoka kwako au linatoka kwa Mwenyezi Mungu?

Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s) akasema: “Naapa kwa yule ambaye hakuna Mola isipokuwa Yeye, jambo hili linatoka kwa Mwenyezi Mungu.” Basi Numan bin Harith Al-Fihri’akaondoka kuelekea kwenye kipando chake huku akisema: “Ewe Mwenyezi Mungu? Ikiwa anayosema Muhammad (s) ni kweli, basi tunyeshee mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.”

Mtu huyu hakuwahi kufika kwenye kipando chake isipokuwa Mwenyezi Mungu alimpiga kwa jiwe kichwani mwake likatokea kwenye njia ya haja kubwa na kumuua palepale. Ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akateremsha aya isemayo: “Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea…”

IMETAYARISHWA NA KITENGO CHA TABLIGH HQ-BILAL MUSLIM MISSION OF TANZANIA KWA, MNASABA WA MAADHIMISHO YA GHADIR KHOUM.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *