MSIKITI WA BILAL UDOE WAFUTURISHA WAKIADHIMISHA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA IMAM ALI (A.S).

 MSIKITI WA BILAL UDOE WAFUTURISHA WAKIADHIMISHA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA IMAM ALI (A.S).

Mamia ya wakaazi wa Dar es salaam kutoka dini na madhehebu mbalimbali wamehudhuria katika hafla ya iftar ya pamoja iliyoandaliwa na msikiti wa Bilal Udoe, ulio chini ya taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania (BMMT)…

Tukio hilo ambalo limeenda sambamba na kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kishahidi cha imam Ali bin Abi talib (a.s) limefanyika April 12, 2023 msikitini hapo, mtaa wa Udoe – Kariakoo, jijini Dar es salaam.

Sheikh Mohammed Mubarak, imamu wa masjid Bilal Udoe alizungumza kuhusu maisha ya imam na kuwahimiza watu wote bila kujali itikadi zao za kiimani kumsoma zaidi imam Ali hususani kupitia kitabu chake cha Nahju Balagha kwani kitabu hiko kina darsa kubwa juu ya masuala ya kiimani, maisha ya kijamii na mambo mengine mengi.

Imam Ali (a.s) ni imam wa kwanza kati ya maimam 12 baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na alikufa shahidi mnamo tarehe 21 Ramadhan, 40 Hijiria kwa kupigwa upanga msikitini wakati wa swala ya alfajiri kutokana na njama za watu waliokuwa na nia ovu dhidi ya uislamu.

Ni utamaduni wa msikiti wa Bilal Udoe kuandaa tukio la namna hii lenye malengo ya kuwaweka pamoja waumini wa madhehebu ya shia ithna asheri na madhebu nyingine za kiislamu na wasiokuwa waislamu malengo yakiwa ni kuimarisha umoja na mshikamano baina ya wanaadamu wote bila kujali itikadi zao za kidini au kimadhehebu.

Kwa niaba ya uongozi wa msikiti wa Bilal Udoe, na BMMT, tunatoa shukrani kwa wote waliofanikiwa kuhudhuria tukio hili muhimu na pia tunatoa shukrani za dhati kwa kila mmoja aliyewezesha kufanikiwa kwa tukio hili kupitia mchango wake wa hali na mali na Mwenyezi Mungu atawalipa wote, in sha Allah!

PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *