Office Hours
Mon-Fri: 08:30am-05:30pm Saturday: 08:30am-01:30pm

BMMT YAADHIMISHA MAULIDI YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) KWA KUSHIKAMANA NA MAADILI, UMOJA NA HUDUMA KWA JAMII NCHINI

DAR ES SALAAM, TANZANIA — Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania (BMMT) imeungana na Waislamu pamoja na jamii kwa ujumla katika kuadhimisha mazazi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) kupitia shughuli mbalimbali za kijamii, kitaaluma na kimichezo zilizofanyika katika maeneo tofauti nchini.

Maadhimisho ya mwaka huu yaliyoongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuishi Maadili ya Mtume (S.A.W.W): Umoja na Huduma kwa Jamii”, yakiwa na lengo la kumuenzi Mtume (s.a.w.w) kwa kuimarisha Akhlaq (tabia njema), kuendeleza elimu na mshikamano wa kijamii.

Hafla Kuu Jijini Dar es Salaam

Hafla kuu ya maadhimisho hayo ilifanyika siku ya Jumamosi, tarehe 19 Septemba 2026, katika Ukumbi wa Unity Hall, Chang’ombe-Temeke, jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na zaidi ya waumini na wageni waalikwa 3,000; ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini na serikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi ambaye ni Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Abbasi Ramadhani Abbas, alisisitiza umuhimu wa umoja katika Umma wa Kiislamu na kutoa wito wa kuondokana na ubaguzi wa kimadhehebu na kiitikadi.

Katika wasilisho la mada kutoka kwa wanazuoni mbalimbali:

  • Dkt. Sheikh Mulaba alizungumzia mabadiliko ya kifikra yaliyojengwa na ujio wa Mtume (s.a.w.w) na umuhimu wa kurekebisha mitaala ya elimu ili kumjenga mwanadamu mwenye maadili.
  • Sheikh Said alieleza nafasi ya Mtume (s.a.w.w) kama rehema kwa walimwengu na kuhamasisha matendo ya huruma katika maisha ya kila siku.
  • Sheikh Hussein Zubeir alibainisha namna Mtume (s.a.w.w) alivyojenga Umma wenye umoja kupitia misingi ya Mu’ākhāt (udugu kati ya Muhajirun na Ansar).

Semina na Shughuli za Kijamii Mikoani

Maadhimisho ya Maulidi ya Mtume (s.a.w.w) yalienea katika kanda na matawi mbalimbali ya BMMT nchini

  • Zanzibar: Tarehe 20 Septemba 2026, BMMT Zanzibar iliandaa semina iliyohusu “Vijana, Uongozi na Maadili” katika Ukumbi wa ZBC Radio Rahaleo. Dkt. Shaaban Al-Battashi (aliyemwakilisha Mufti Mkuu wa Zanzibar) pamoja na wawakilishi wa Jeshi la Polisi walishiriki kutoa nasaha kwa wanafunzi wa vyuo na shule za sekondari kuhusu kukabiliana na kuporomoka kwa maadili.

  • Sikonge (Tabora): Maadhimisho yalienda sambamba na maonesho ya taaluma kwa wanafunzi wa madrasa na vituo vya watoto wadogo (Nursery), yakihusisha pia madrasa za ndugu zetu Ahlus Sunnah katika kuimarisha mshikamano.
  • Moshi (Kilimanjaro): Mashindano ya BMMT Moshi Maulid Cup 2026 yalihusisha timu 12 kutoka wilaya mbalimbali, ambapo timu ya Kijana Kwanza FC iliibuka mshindi wa kwanza na kutunukiwa kikombe, seti ya jezi na zawadi ya fedha.

Shukrani na Wito

BMMT inatoa shukrani za dhati kwa viongozi wa dini, serikali, masheikh, wadau wa elimu, na waumini wote walioshiriki kufanikisha maadhimisho haya. Shukrani za pekee zinakwenda kwa wafadhili na wahisani, ikiwemo taasisi ya The Mainstay Foundation, kwa mchango wao mkubwa uliyowezesha kufanikiwa kwa programu hizi.

Taasisi inawasihi Waislamu na jamii kwa ujumla kuendelea kuweka katika vitendo mafundisho ya Sīra ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlulbayt (a.s.) kwa kudumisha amani, udugu, na huduma kwa viumbe wote.

  • Morogoro (Kanda ya Kati): Semina ya Maulidi ilifanyika katika Ukumbi wa Atubellah ikihudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa BMMT, Ndg. Hafidh Mansour, viongozi wa serikali, vyama vya siasa na viongozi wa kidini. Mada kuu zilizingatia uadilifu katika uongozi na utoaji wa huduma kwa jamii. 
  • Mwanza: Tawi la BMMT Mwanza liliandaa semina iliyofanyika Masjid Imam Hussein (a.s.), Nyamhongolo. Mbali na mawaidha kutoka kwa Samahat Sheikh Hussein Zubeir, mashindano ya mpira wa miguu (Maulid Cup) yaliandaliwa ambapo timu ya Shia iliibuka mshindi.

About the Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You may also like these

{title}