Semina ya siku tatu imeunganisha elimu ya dini, stadi za mawasiliano, uongozi na matumizi ya maadili ya teknolojia ili kuimarisha kazi ya tabligh katika vituo vya BMMT nchini.
Dar es Salaam, 19 Julai 2026 — Taasisi ya The Bilal Muslim Mission of Tanzania (BMMT), kupitia Kamati ya Wanawake, imeendesha Semina ya Kuwajengea Uwezo Mubalighat 44, kutoka kanda mbalimbali za taasisi nchini.
Semina hiyo ilifanyika kuanzia Ijumaa, tarehe 17 hadi Jumapili, tarehe 19 Julai 2026 katika Hawzat Maasoomat (a.s.), Ubungo–Mabibo, Dar es Salaam. Lengo lake lilikuwa kuimarisha uwezo wa washiriki katika elimu ya dini, uwasilishaji, uongozi, uratibu wa majalisi na matumizi ya maadili ya mitandao ya kijamii katika kuendeleza kazi ya tabligh.
Kwa muda wa siku tatu, washiriki walipitiwa mafunzo ya kina yaliyochanganya mihadhara, majadiliano, kazi za vikundi, tafakuri na mazoezi ya vitendo. Mfumo huo uliwapa nafasi ya kujifunza, kushirikishana uzoefu na kuandaa mikakati ya kutumia maarifa waliyoyapata katika vituo na jamii wanazozihudumia.
Tabligh yenye elimu, ikhlasi na hekima
Semina ilifunguliwa rasmi na Makamu Mwenyekiti wa BMMT, Sheikh Abdul Wahidi. Katika nasaha zake kwa washiriki, alisisitiza umuhimu wa kuwa na nia safi, elimu sahihi na dhamira ya dhati katika kutekeleza majukumu ya tabligh.
Aliwakumbusha Mubalighat kuwa jukumu la kufikisha mafundisho ya Uislamu ni amana inayohitaji uadilifu, unyenyekevu, subira na mwenendo mwema. Alisisitiza pia kuwa Mubaligha hatakiwi kuwa mzungumzaji pekee, bali anapaswa kuwa mwalimu, mlezi wa maadili na kiungo cha umoja katika jamii.
Mafunzo ya siku ya kwanza yalijikita katika historia na ujumbe wa Karbala, umuhimu wa Muharram pamoja na nafasi ya majalisi katika kuhifadhi na kufikisha mafundisho ya Uislamu. Washiriki walijifunza namna ya kuunganisha historia ya Karbala na changamoto za maisha ya kila siku, hususani katika kulinda haki, kuimarisha ucha-Mungu na kujenga jamii yenye uadilifu na huruma.
Nafasi ya wanawake katika kuhifadhi na kueneza ujumbe wa Karbala nayo ilipewa uzito maalumu. Kupitia mafunzo yanayotokana na maisha na msimamo wa Sayyida Zaynab (a.s.) pamoja na wanawake wengine wa Karbala, Mubalighat walihimizwa kutumia elimu, subira, ujasiri na ufasaha katika kuutetea ukweli.
Kuandaa majlisi yenye mpangilio na athari
Katika upande wa uandaaji wa maudhui, washiriki walifundishwa muundo bora wa majlisi, kuanzia kisomo cha ufunguzi, utangulizi, mhadhara mkuu na sehemu ya masaibu mpaka hitimisho, dua na matangazo.
Usimamizi mzuri wa muda ulisisitizwa ili kila sehemu ya majlisi ipewe nafasi inayostahili bila kupunguza ubora wa ujumbe au kuwachosha wasikilizaji. Mubalighat walihimizwa kuandaa mihadhara kwa kutegemea Qur’ani Tukufu, Hadithi na riwaya sahihi, pamoja na kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kuwasilisha jambo kwa umma.
Mafunzo hayo hayakuishia katika nadharia, bali kila mshiriki aliandaa na kuwasilisha utangulizi wa majlisi kwa dakika tano, kisha akapokea mrejesho kutoka kwa wawezeshaji na washiriki wenzake. Zoezi hilo liliwasaidia kutambua maeneo ya kuboresha katika mpangilio wa mada, matumizi ya muda, sauti na namna ya kuifikia hadhira.
Ujumbe mmoja kwa hadhira tofauti
Siku ya pili ya semina ilijikita katika stadi za kuzungumza mbele ya hadhira na kuendesha majalisi kwa makundi yenye mahitaji tofauti. Washiriki walifanya mazoezi ya matumizi sahihi ya sauti, lugha ya mwili, ukimya, hisia na mawasiliano yasiyo ya maneno.
Walijifunza pia mbinu za kudhibiti wasiwasi, kujenga kujiamini na kutumia hisia kwa kiasi kinachofaa, hususani wakati wa kusimulia masaibu. Msisitizo uliwekwa katika kudumisha ukweli, utulivu na staha ili ujumbe uweze kugusa nyoyo bila kupoteza uhalisia au kuvuka mipaka ya maadili ya Kiislamu.
Kwa kutambua kuwa hadhira hutofautiana, Mubalighat walipitiwa mbinu za kuandaa majalisi za wanawake, vipindi vya vijana na programu za Muharram kwa watoto. Mafunzo yalionesha kuwa kila kundi linahitaji lugha, mifano na mbinu za ufundishaji zinazolingana na umri, mazingira na kiwango chake cha uelewa.
Aidha, washiriki walijengewa uwezo wa kujibu maswali magumu kwa hekima, kusikiliza kwa makini, kutatua migogoro na kuheshimu tofauti za mila na tamaduni katika jamii. Walikumbushwa kuepuka majibu yasiyo sahihi yanayoweza kuleta mgawanyiko au kupunguza heshima ya majlisi.
Kila mshiriki aliwasilisha majlisi mfupi wa dakika kumi na kupokea tathmini kuhusu mpangilio wa mada, matumizi ya sauti, usimamizi wa muda na ushirikishwaji wa hadhira.
Uongozi na uratibu wa programu
Siku ya tatu iliunganisha elimu ya dini na uhalisia wa utekelezaji wa programu. Mubalighat walijifunza namna ya kuandaa ukumbi wa majlisi, kupanga ratiba na majukumu, kusimamia mfumo wa sauti, kuratibu washiriki na kuhakikisha usalama pamoja na usafi wa mazingira.
Mafunzo hayo yalionesha kuwa mafanikio ya programu hayapimwi kwa ubora wa mihadhara pekee, bali pia kwa nidhamu ya maandalizi, ushirikiano wa timu na namna wageni na washiriki wanavyopokelewa.
Katika mada ya uongozi na uratibu, washiriki walikumbushwa umuhimu wa kushauriana, kuheshimiana na kuthamini mchango wa wanaojitolea. Ugawaji mzuri wa majukumu na mawasiliano yenye ufanisi vilitajwa kuwa msingi wa kupunguza migongano, kuimarisha uwajibikaji na kuwezesha kila mshiriki kutekeleza jukumu lake kwa ufanisi.


Mitandao ya kijamii kama nyenzo ya tabligh
Katika kuendana na maendeleo ya teknolojia, Ndugu Idrissa Tarimo aliwasilisha mada kuhusu matumizi salama kuhusue maadili ya mitandao ya kijamii katika kufikisha ujumbe wa Uislamu.
Mubalighat walijifunza namna ya kutambua taarifa za kweli, na uzushi na propaganda za mitandaoni. Walipatiwa pia mwongozo wa kuandaa taarifa fupi za shughuli kutoka katika vituo vyao na kuchagua picha pamoja na maudhui yanayolinda heshima, faragha na stara.
Somo hilo liligusia changamoto za unyanyasaji wa kimtandao na umuhimu wa kutumia majukwaa ya kidijitali kwa uwajibikaji. Teknolojia ilielezwa kuwa nyenzo yenye manufaa makubwa katika tabligh ikiwa itatumika kwa usahihi, adabu na kuzingatia athari za maudhui kwa jamii.
Mafunzo kugeuzwa kuwa vitendo
Kabla ya kufungwa kwa semina, washiriki waliandaa mipango ya utekelezaji wa majalisi za Muharram katika maeneo yao. Walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano na jamii, kulea kizazi kijacho cha Mubalighat na kufuatilia maendeleo ya shughuli za tabligh katika kila kanda.
Semina ilifungwa rasmi na Sheikh Abdul Wahidi kwa niaba ya Mwenyekiti wa BMMT. Katika hafla hiyo, alipokea taarifa iliyowasilishwa na washiriki na kuunga mkono pendekezo la kufanya mafunzo hayo kuwa endelevu, angalau mara mbili kwa mwaka.
Aliwahimiza Mubalighat kurejea katika vituo vyao wakiwa na maarifa mapya, nia thabiti, moyo wa ushirikiano na uwajibikaji katika kuitumikia jamii. Vyeti vya ushiriki vilitolewa kwa Mubalighat wote 44 kabla ya semina kuhitimishwa kwa dua.
BMMT inatoa shukrani kwa uongozi wa taasisi, Kamati ya Wanawake, wawezeshaji hususani Dada Maysara Ally, Dada Hytham A. Tajir, Dada Nyembezi Mbano, Sheikh Jaffery A. Mwazoa, Ndugu Hafidh Mansour na Ndugu Idrissa Tarimo, pamoja na washiriki wote kwa mchango na kujitoa kwao katika kufanikisha semina hiyo.
Hatua inayofuata ni kuendeleza mafunzo ya mara kwa mara, kufuatilia utekelezaji wa mipango ya kila kanda na kuimarisha mtandao wa Mubalighat wenye kujifunza, kushirikiana na kuwalea wengine.





