KIFO CHA MTUME MUHAMMAD (S) – MKONO WA POLE KWA ULIMWENGU WOTE.

 KIFO CHA MTUME MUHAMMAD (S) – MKONO WA POLE KWA ULIMWENGU WOTE.

Wanahistoria wa Kiislamu wametofautiana kuhusu tarehe aliyofariki Mtume Muhammad (s) kuwa ni mwezi 12 mfungo sita mwaka wa 11 tangu kuhama Makkah, au ni mwezi 28 mfungo tano mwaka huo huo wa 11. Muhimu siyo kutaka kufahamu ni ipi tarehe sahihi kati ya hizo mbili, bali wengi wameafikiana kuwa kifo cha Mtume (s) kilitokea mwaka wa 11 hijiriyah.

Makala haya mafupi yanalenga kudondoa baadhi ya sifa muhimu za Mtume Muhammad (s) aliyetumwa kwa walimwengu wote.

Ujumbe aliokuja nao Mtume (s) ulikuwa ni ujumbe kwa ajili ya wanadamu wote na sio kwa taifa au kabila fulani tu. Mwenyezi Mungu anasema: “Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mwenye mbashiri, na mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui.” Qur 34:28

Katika kufafanua kuwa Mtume (s) ametumwa kwa mataifa na makabila yote anasema: “…nimepewa mambo matano, na siyasemi haya kwa majivuno. Nimetumwa kwa weupe na weusi…”

Mtume wa rehma

Kazi ya kubashiria watu mema na kuwaonya maovu ni kazi nzito na inahitaji maandalizi muhimu na maalum kwa mbashiri na muonyaji. Bila shaka sifa ya huruma uvumilivu kujitolea ni miongoni mwa sifa zinazohitajika kwa mtu kama huyu.

Mwenyezi Mungu anasema kumwambia Mtume Muhammad (s) kwamba: “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” Qur 21:107

Hapana shaka kuwa watu wote katika ulimwengu huu Waislamu na wasiyokuwa Waislamu wanahitajia kupata rehma au huruma kutoka kwa Mtume wetu Muhammad (s) ambaye alibeba jukumu la kuhakikisha rehma hiyo anaipata kila mwanadamu hapa ulimwenguni.

Ndiyo maana mwanzoni tu mwa kudhihiri kwa Utume wake aliwapelekea barua wafalme wa dola kubwa za wakati ule akiwemo Kisra na Najashi akawaita wao na watu wao kwenye rehma hii ambayo ni kwa ajili ya walimwengu wote.

Mpole mwenye huruma

Mwenyezi Mungu anamsifu Mtume wetu (s) kwa sifa ya upole na huruma aliposema: “Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.” Qur 09:128

Na katika aya nyingine anasema: “Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee msamaha,…” Qur 03:159

Kwa ujumla kila kiongozi anatakiwa kupamboka kwa sifa hizi zilizotajwa ndani ya aya hizo hapo juu.

Kiongozi anatakiwa awe mwenye kutambua na kujali matatizo ya wale anao waongoza, kama ambavyo anatakiwa mpole na mwenye kusamehe kwa watu wa chini yake. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa tabia na mwenendo wa Mtume wetu Muhammad (s).

Kwa mujibu wa aya hizo hapo juu, kiongozi hatakiwi kuwa mkali, mwenye moyo mgumu na msusuavu wa tabia kwani hali hiyo inaweza kuwafanya watu wakose amani na pengine kumkimbia kiongozi wa aina hiyo. Imam Ali (a) anasema: “Nyenzo ya uongozi ni kuwa na kifua kipana.”

Kwa hakika Mtume wetu Muhammad (s) alitumwa kwa wanadamu wote kuhubiri huruma na tabia njema ili kuwaepusha dhidi ya udhalima, ufisadi, udanganyifu na tamaa. Tukiwa tunakumbuka kifo cha Mjubme huyu wa Mwenyezi Mungu, tunapaswa kutambua kuwa yeye ni kiigizo chetu kikubwa katika maisha yetu binafsi na pia mahusiano na wengine, wawe Waislamu au wasiwe Waislamu.Tukamilishe kwa kunukuu kauli ya Mtume wetu (s) pale aliposema: “Wahurumieni waliyoko ardhini nanyi atakuhurumieni aliyeko mbinguni.

 

IMETAYARISHWA NA

KITENGO CHA TABLIGH

BILAL MUSLIM MISSION OF TANZANIA (BMMT) MAKAO MAKUU

Sept 24, 2022

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *