MSKITI WA UDOE WAFUNGULIWA BAADA YA KUFANYIWA MABORESHO


Alhamdullillah, tumefanikiwa kufungua Msikiti wa Udoe baada ya kufanyiwa maboresho.
Hafla ya ufunguzi wa msikiti iliambatana na maadhimisho ya kumbukumbu ya mazazi ya Imam Hussein, Hadhrat Abbas na Imam Ali Zainul Abidiina (a) waliozaliwa katika mwezi kama huu (Shaaban)
Mwenyekiti wa Africa Federation (AFED) Alhajj Shabiri Najafi ndiye aliyekuwa mgeni wa heshima, wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamo Mwenyekiti wa AFED, Alhajj Aunali Khalfani, Mwenyekiti Bilal Muslim Mission of Tanzania (BMMT) Alhajj Hussein Karim pamoja na Makamo wake, Alhajj Abdul-Wahid Zakaria sambamba na waumini wengine.
Hafla hiyo ilianza baada ya Swalatul Maghrib na ilitanguliwa na dua’a ya kila Alkhamis (Dua’a Kumayl), Ufunguzi wa hafla kwa kisomo cha Qur-an, mada mbalimbali zikiwemo historia za mskiti huo, kufunga hafla kwa kisomo cha ziara mbalimbali na baadae sadaka ya chakula cha pamoja.
Katika hotuba yake Mwenyekiti wa AFED, Alhajj Shabiri Najafi amesema amefurahishwa na hali ya Mskiti baada ya maboresho na kutoa neno la shukrani kwa wafadhili wa zoezi hilo.
Alhajj Najafi pia amewatolea mwito waumini kushiriki katika harakati za hisani kulingana na kipato chao wakitegemea malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani jambo hilo ni la wajibu wa kila mmoja katika sisi.
Hotuba ya Mwenyekiti wa AFED ilitanguliwa na wazungumzaji wengine akiwemo Sheikh Swahib Rashid (Sheikh Mkuu BMMT – Pwani na Kusini) na Makamo Mwenyekiti wa BMMT, Alhajj Abdul Wahid Zakaria ambaye alitoa historia na kukumbuka malengo ya ujenzi wa Mskiti huo ikiwemo kuleta mshikamano baiana ya jamii mbalimbali za Kiislamu.
Katika upande mwingine Alhajj Abdul-Wahid alimshukuru na kumpongeza Ndugu Ain Sheriff pamoja na timu yake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kusimamia haraka za mskiti huo…
Bilal Muslim Mission of Tanzania inamshukuru Mwenyekiti wa AFED, Alhajj Shabiri Najafi kwa kukubali kuwa mgeni wa heshima na kushiriki katika hafla ya ufunguzi wa msikiti baada ya maboresho pia inatoa shukran za dhati kwa wafadhili wa maboresho ya mskiti huo na kila mmoja aliyeshiriki kufanikisha shuguli hii.
Bilal pia inatoa mwito kwa waumini kuendelea kushiriki kwenye harakati za hisani kama hizi na nyingine ambazo bado zinahitajika ili kuupeleka mbele Uislamu wetuna malipo ni makubwa mbele za Mwenyezi Mungu.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA HAFLA YA UFUNGUZI WA MSKITI WA UDOE






