Dar es Salaam, Tanzania – 7 Juni 2026
The Bilal Muslim Mission of Tanzania imefanikiwa kuandaa na kuendesha kwa mafanikio makubwa maadhimisho ya Eid Ghadeer yaliyofanyika tarehe 7 Juni 2026 katika Ukumbi wa Unity Hall, Chang’ombe, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya wanavyuo wa 2,500 walihudhuria kutoka vyuo vikuu mbalimbali.

Maadhimisho hayo yalibeba kaulimbiu isemayo: “Ghadeer; Ujumbe wa Uongozi na Mustakabali wa Umma”, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi katika kukuza uelewa sahihi wa mafundisho ya Kiislamu, kuimarisha maadili ya uongozi bora na kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii yenye maendeleo na ustawi.
Katika kongamano hilo, washiriki walipata fursa ya kusikiliza mada mbalimbali zilizowasilishwa na wanazuoni mashuhuri. Miongoni mwao alikuwa Sheikh Hussein Zuber, ambaye alitoa ufafanuzi wa kina kuhusu tukio la Ghadeer, akibainisha nafasi yake katika historia ya Uislamu na umuhimu wake katika kuendeleza maadili ya uongozi wa haki, uadilifu na uwajibikaji.
Aidha, Sheikh Dkt. Abdulrazack Amir aliwasilisha mada kuhusu falsafa za utawala na uongozi katika Uislamu, akisisitiza umuhimu wa viongozi kuwa na maono, uadilifu, elimu na dhamira ya dhati katika kuwatumikia wananchi na kulinda maslahi ya umma.
Sheikh Hussein Zubeir Sheikh,Dkt Abdulrazack Amir
Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa Chief Kadhi ikutoka Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) na Mjumbe wa Baraza la Maulamaa, Sheikh Ali Ngeruko, ambaye katika hotuba yake alisisitiza kuwa mafunzo na malengo yanayotokana na tukio la Ghadeer yanapaswa kutafsiriwa kwa vitendo katika maisha ya kila siku, badala ya kubaki katika maneno na nadharia pekee.
Sheikh Ngeruko alihimiza vijana kujijenga kielimu, kiakhlaki na kiuchumi ili waweze kuwa viongozi bora wa kesho. Alibainisha kuwa ni wajibu wa vijana kutambua nafasi yao katika kusimamia nyadhifa mbalimbali za uongozi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa na Umma kwa ujumla. Vilevile, aliwasisitiza kufanya kazi kwa bidii na kutumia fursa zilizopo kwa njia halali ili kujijengea uwezo wa kiuchumi na kujitegemea.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa The Bilal Muslim Mission of Tanzania, Sheikh Abdul Wahid Abdallah, alipotoa neno la shukrani, aliwashukuru kwa dhati washiriki wote waliohudhuria maadhimisho hayo na kuchangia kufanikisha tukio hilo kubwa. Alieleza kuwa mada zilizowasilishwa zina uwezo wa kubadilisha mustakabali wa maisha ya vijana iwapo zitafanyiwa kazi kwa vitendo na kuzingatiwa katika maisha yao ya kila siku.
Aidha, aliwahamasisha vijana kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa, ikiwemo ufadhili wa masomo, mafunzo ya maendeleo ya vijana pamoja na mikopo ya kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kujenga maisha yenye heshima na ustawi.
Maadhimisho ya Eid Ghadeer ya mwaka huu yameendelea kudhihirisha dhamira ya The Bilal Muslim Mission of Tanzania ya kuwaandaa vijana wenye elimu, maadili, uwezo wa kiuongozi na uzalendo, ili waweze kuwa nguzo imara ya maendeleo ya Umma na Taifa kwa ujumla.
“Hakika jamii bora hujengwa na vijana wenye maono, maarifa, maadili mema na utayari wa kuitumikia jamii yao kwa uaminifu na uadilifu.”







