MAADHIMISHO YA ASHURA YAIMARISHE UMOJA NA SIYO MGOGORO BAINA YA MADHEHEBU YA KIISLAMU

 MAADHIMISHO YA ASHURA YAIMARISHE UMOJA NA SIYO MGOGORO BAINA YA MADHEHEBU YA KIISLAMU

Kwa karne nyingi tukio la mauaji dhidi ya imam Husein (a) na wafuasi wake huko Karbala, limekuwa likipotoshwa kutoka kwenye uhalisia wake na kutajwa kuwa ni moja kati ya sababu za kuwepo kwa mifarakano katika jamii ya Waislamu.
Maadui wa Uislamu kwa miaka mingi wameendelea kueneza uongo kuwa, kumbukumbu na maadhimisho ya Ashuraa ni vuguvugu la madhehebu fulani dhidi ya madhehebu mengine ya Kiislamu. Aidha wanadai kwamba, mauaji hayo yalitokana na uasi wa kimadhehebu dhidi ya mamlaka ya zama hizo iliyokuwa imejengwa kwenye misingi ya madhehebu tofauti na wahusika waliyouliwa na ambao kwa leo wanaungwa mkono na hawa wanaoadhimisha tukio hilo mwaka kwa mwaka.

Hakika ya ukweli ni tofauti na hivyo ilivyoenezwa kuanzia siku hizo mpaka sasa. Kwa mujibu wa historia ni kwamba, imam Hussein (a) ambaye ndiye muhusika mkuu kwa upande mmoja, aliweka bayana msimamo na lengo lake la kutoka dhidi ya mamlaka hiyo.

Historia inanukuu maneno bayana ya imam Husein (a) kama kauli mbiu yake wakati akiagana na nduguye kwa jina akiitwa Muhammad al Hanafiyyah anasema: “Kwa hakika mimi sikutoka kwa sababu ya ujeuri wala majivuno wala kufanya ufisadi wala dhulma. Bila shaka nimetoka kwa ajili ya kuurekebisha umma wa Babu yangu. Nataka niamrishe mema na nikataze maovu. Yeyote mwenye kuniitikia kwa kuufuata ukweli huu, Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kustahiki mno katika ukweli. Na atakayenipinga juu ya hili, basi nitasubiri mpaka hapo Mwenyezi Mungu atakapohukumu kwa haki kati yangu na watu hao, kwani yeye ndiye hakimu bora mno.”

Ndugu msomaji! Ukiyarejea maneno haya kwa makini utayakuta yanawakilisha maslahi ya Uislamu na ni ujumbe wa Kiislamu uliyobebwa na imam Husein (a) ambao ni urithi adhimu kutoka kwa babu yake, Mtukufu Mtume (s).
Kwa mintarafu hiyo, njia bora ya kuenzi lengo hili la imam Husein (a) na tukio lote kwa ujumla, ni kupatikana kwa umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu na siyo kuwatenganisha.

Zaidi ya hapo, kauli mbiu hii ya imam Husein (a), ilipaswa kuwaweka karibu Waislamu na kuwapa fursa ya kushauriana wao kwa wao kuhusu dini yao hasa katika uwanja wa kuamrishana mema na kukatazana maovu. Aidha ni fursa nzuri ya kujadili na kuyapatia ufumbuzi mambo mbalimbali yanayoonekana kuwa ni kikwazo cha ushirkiano, maendeleo ikiwemo elimu na mengineyo muhimu ya kijamii.

IMAM HUSEIN (A) HAKUPIGANIA MADHEHEBU
Fikra ya kumfanya imam Husein (a) kuwa ni mwakilishi wa madhehebu fulani  ni upotoshaji wa wazi na ni madai yasiyokuwa na msingi.

Kila mmoja wetu anapaswa kufahamu kuwa, imam Husein bin Ali (a) hakuwa Shia, bali alikuwa Muislamu na pia kiongozi wa Waislamu. Wito wake aliyoulingania ni wito wa Uislamu na si kinyume cha hivyo.
Kuyasawiri na kulifanya tukio la Karbala kuwa ni mgongano au mgogoro kati ya madhehebu ya Kiislamu ni uongo, na si sahihi kwa mujibu wa historia.

Kwa mukhtasari twaweza kusema dhamira ya uzushi huo inalenga kuwavuruga Waislamu na kuwafanya wasielewane na waendelee kugawanyika na hatimaye nguvu zipotee.
Ukweli wa mambo ni kwamba, kilichotokea huko Karbala mnamo mwaka wa 61 (a.h), ni mapambano kati ya haki na batili, ambapo haki iliwakilishwa na wanaoshikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu.

MAKOSA YA UFAHAMU YANAENDELEA
Katika zama zetu hizi, bado ufahamu wa kimakosa unaendelea kuhusu dhamira na malengo ya muhanga wa imam Husein (a) na wafuasi wake. Mpaka sasa bado kuna watu miongoni mwa Waislamu wanaofanya kila njia kupotosha uhalisia wa tukio hili kwa maana ya chanzo chake halisi katika historia ya Uislamu. Pengine bila kufahamu kwamba, hivyo wanavyofanya ni moja kati ya njia za kuutia nguvu mgawanyiko wa kimadhehebu uliyopo baina ya Waislamu.

Tunasema hivyo kwa sababu, historia inatueleza wazi kwamba, imam Husein (a) alitoka dhidi ya Yazid bin Muawiya (khalifa wa zama hizo) kwa lengo la kuulinda umma wa Kiislamu na alitamka bayana mwanzoni mwa safari yake kuelekea Karbala kama tulivyoashiria hapo juu.

Imam Husein (a) hakutosheka tu na kubainisha lengo la kutoka kwake bali alieleza wazi mwenendo na tabia ya Yazid kwamba hakuwa na maadili ya dini akasema: “…na Yazid ni mtu fasiq (muovu) anayekunywa mvinyo (ulevi), anaua watu wasiyokuwa na hatia, na uovu wake anaufanya wazi wazi (mchana kweupe). (Kwa hali hiyo) mtu kama mimi hawezi kula kiapo cha utii (kwake).”

Hali na mazingira ya umma kwa ujumla zama hizo iligubikwa na vitendo vya aina hii, kama isemwavyo kwamba, watu hufuata nyendo za watawala wao. Hivyo basi, dhamira na shakhsiya ya imam Husein bin Ali (a) haikuridhia kuona haya yanafanyika kisha kukaa kimya.

Mwislamu anao uhuru na wajibu wa kusoma historia ili kufahamu zaidi na kwa undani ili kufahamu kwa undani sababu kadhaa wa kadhaa zilizomfanya imam Husein (a) kuamua kutoka dhidi ya mamlaka hayo yaliyokuwa yakitawala wakati huo. Ukweli ni kwamba uharibifu katika dini ulifikia kiwango ambacho hapakuwa na namna isipokuwa kupatikana watu wa kujitolea muhanga kuihami dini ya Mwenyezi Mungu.

Kwa msingi huu basi, wito wetu kwa jumuiya ya Waislamu ni kwamba, tukio la Ashuraa linapaswa kuwa ni mnasaba wa kuwaunganisha Waislamu na siyo kuwagawa kwa kuwa asili yake imejengwa juu ya msingi wa kuamrisha mema na kukataza maovu.
Hilo linawezekana iwapo tu lengo na madhumuni ya mnasaba huu yataelezwa na kufafanuliwa kwa kuzieleza sababu halisi zilizopelekea kutokea kwake.
Tuungane pamoja
Mwisho, tunaitumia fursa hii kukualikeni nyote bila kujali tofauti zetu za dini au madhehebu tuungane sote katika maombolezo ya kuikumbuka siku ya msiba mkubwa wa kifo cha mjukuu wa Mtume (s) aliyeuliwa kwa dhulma akitetea Uislamu, Ubinadamu na Maadili mema.

IMETAYARISHWA NA KITENGO CHA TABLIGH THE BILAL MUSLIM MISSION OF TANZANIA HQ

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *