UZINDUZI WA MSIKITI MPYA WA BILAL MWANZA (IMAM HUSEIN CENTRE), NYAMUHONGOLO – MWANZA.

 UZINDUZI WA MSIKITI MPYA WA BILAL MWANZA (IMAM HUSEIN CENTRE), NYAMUHONGOLO – MWANZA.

Tarehe 2 Machi 2024 (20 Shab’an 1445 AH), Bilal Muslim Mission of Tanzania (BMMT) ilifanya uzinduzi wa Msikiti wa Bilal Mwanza na Kituo cha Imam Hussein, hii ni moja ya vituo vikubwa zaidi vya Bilal nchini Tanzania. Sherehe hiyo ilipambwa na uwepo wa Alhaj Mohamedraza Badami na Syed Mohammad Ansar Hussein Naqvi kama wawakilishi wa “Spirit of Hussein” ambao ndio wafadhili wa mradi huo. Alikuwepo pia, Syed Ali Raza Ansar Hussein Naqvi na watoto wawili wa marehemu Syed Hassan Abbas Naqvi, ambao ni Syed Maitham na Syed Zainulabideen waliosafiri kutoka Uingereza na Kanada kuhudhuria hafla hii maalum.

Mwenyekiti wa Afrika Federation (AFED), Alhaj Amine Nassor aliyesafiri kutoka Reunion aliambatana na Makamu Mwenyekiti Alhaj Aunali Khalfan. Viongozi wengine waliokuwepo ni; Naibu Kadhi Mkuu wa BAKWATA Sheikh Ally Hamisi Ngeruko, Sheikh Mkuu wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza Alhaj Hassan Kabeke, Mwenyekiti wa Bodi ya Nyumba ya AFED Alhaj Akil Hirji, Mwenyekiti wa Bodi ya Bilal Alhaj Mohamed Hemani, Mwenyekiti wa AFTAB Alhaj Sajjad Walji, Mwenyekiti wa Bilal Tanzania Alhaj Hussein Karim. Mwenyekiti wa Bilal Kanda ya ziwa, Alhaj Sibtain Meghjee, Mwenyekiti wa Tawi la Bilal Bukoba Alhaj Mohamed Manji, Mwenyekiti wa Jamaat Mwanza Alhaj Arshad Jetha, Mratibu wa Mradi wa AFED Ndugu. Mohamed Moledina, Maimamu na Masheikh kutoka Vituo mbalimbali vya Bilal Tanzania na wageni kutoka taasisi na mashirika mbalimbali pamoja na wanajumuiya kutoka Mwanza.

Kiwanja hicho chenye ukubwa wa ekari 2.3 eneo la Nyamhogoro jijini Mwanza kilitolewa na Alhaj Murtaza Alloo wa Mwanza kwa Bilal Muslim Mission of Tanzania. Uwekaji wa jiwe la msingi ulifanywa na Mwenyekiti wa AFED, Alhaj Amine Nassor tarehe 28 Oktoba 2022 na baada ya hapo ujenzi ulianza chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Bilal Kanda ya Ziwa, Alhaj Sibtain Meghjee.

Mradi huo ulikabidhiwa kwa Bodi ya Maendeleo ya Makazi ya AFED mnamo Oktoba 2023 ili kuendelea na kazi za ujenzi na umaliziaji hadi kukamilika kwake. Mradi huo ulikuwa chini ya usimamizi wa Mratibu wa Mradi wa Bodi ya Maendeleo ya Makazi, Ndugu. Mohamed Moledina, ambaye pamoja na timu ya vibarua 16 kutoka jijini Dar es Salaam walifanya kazi kubwa kuhakikisha mradi unakamilika kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kurahisisha jumuiya ya Bilal kufanya Ibada kwa utulivu katika msikiti huo mpya wenye miundombinu bora.

Mradi huo ulifadhiliwa na “Spirit of Hussein” kwa niaba ya Marhum Syed Hassan Abbas Naqvi na Marhum Masumali Mohamedali Bandali.

Kabla ya kuanza kwa hafla ya uzinduzi wa Msikiti, Surah Yasin ilisomwa na mwanafunzi wa hawza na kufuatiwa na Khitma ya Qur’ani Tukufu iliyosomwa na Samahat Sheikh Abdulwarith wa Ilemela kwa ajili ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, ambaye kwa huzuni aliuaga ulimwengu huu tarehe 29 Februari 2024 na kuzikwa tarehe 2 Machi 2024 huko Zanzibar. Mwenyezi Mungu (swt) ampe maghfirah, na amani ya milele, Aamiyn.

Hafla hiyo ilianza kwa hotuba ya ukaribisho iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bilal Kanda ya Ziwa, Alhaj Sibtain bhai Meghjee na kufuatiwa na hotuba muhimu ya Mwenyekiti wa Bilal Muslim Mission of Tanzania, Alhaj Hussein Karim.

Katika hotuba yake, Alhaj Hussein bhai Karim alitoa historia fupi iliyopelekea uamuzi wa Bilal na AFED kujenga Msikiti na miundombinu mingine kama Madresah, Shule ya awali nk ambavyo vilikosekana Mwanza kwa miaka mingi. Alibainisha kuwa Makamu Mwenyekiti wa AFED Alhaj Aunali Khalfan alikuwa na mchango mkubwa na kutoa chachu ya ujenzi wa msikiti wa Bilal jijini Mwanza. Hussein Bhai alisisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na msikiti pamoja na utunzaji wa msikiti huo. Alisema wafadhili hao wamepanga kuendelea na maendeleo ya awamu ya 2 ya mradi huo ambayo ni pamoja na jengo la ofisi, makazi ya waalimu na walezi, uzio pamoja na kituo cha afya. Aliwashukuru wafadhili kwa msaada wao.

Naibu Kadhi Mkuu wa BAKWATA Sheikh Ally Ngeruko naye alishukuru kwa mchango huo adhimu na kuwataka wakazi wa Mwanza kutumia miundombinu hiyo kikamilifu. Alipendekeza kufanyike programu za kuwaelimisha watoto wadogo, vijana wakubwa juu ya masomo ya maisha, elimu ya ndoa kwa wanandoa wachanga pamoja na huduma za upatanisho ili kusaidia kuokoa ndoa.

Mwenyekiti wa AFED, Alhaj Amine bhai Nassor, katika hotuba yake iliyotafsiriwa kwa Kiswahili na Makamu Mwenyekiti wa AFED, Alhaj Aunali Khalfan, alisema Msikiti na Kituo cha Bilal ni ndoto ya Marhum Syed Hassan Abbas Naqvi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa zamani wa AFTAB. Yeye pamoja na Makamu Mwenyekiti wa AFED Alhaj Aunali Khalfan walikuwa waanzilishi wakuu wa mradi huu wa kupongezwa.

Aliipongeza na kuishukuru familia ya Marhum Syed Hassan Abbas Naqvi na familia ya Marhum Alhaj Masoomali Mohamedali Badami kwa kufadhili mradi huu wa Msikiti na Kituo ambapo shughuli zote za kidini na elimu ya Kiislamu zitafanyika.

Alhaj Amine bhai Nassor aliishukuru Bodi ya Maendeleo ya Makazi ya AFED chini ya uongozi mahiri wa Alhaj Akil Hirji kwa ari yake kubwa na kujitolea aambapo matokeo yake tunayashuhudia. Aliwapongeza sana kwa juhudi zao bila kuchoka kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kabla ya muda uliopangwa.

Alitoa shukrani zake kwa Alhaj Sibtain bhai Meghjee kwa ushirikiano na kujitolea kwake. Pia alimshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bilal, Alhaj Mohamed bhai Hemani kwa mwongozo na msaada wake. Alimshukuru Alhaj Hussein bhai Karim, Mwenyekiti wa Bilal Muslim Mission of Tanzania kwa kufanya kazi bega kwa bega na Bodi ya Maendeleo ya Makazi ya AFED kwa kujitolea na bidii kubwa. Pia alishukuru uwepo wa wale wote waliotoa muda wao kuwa sehemu ya Sherehe hiyo.

Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, Syed Muhammad Naqvi alihutubia kwa lugha ya Kiswahili. Alieleza kuwa Spirit of Hussein ni shirika la hisani ambalo linaamini katika kutoa michango chanya kote ulimwenguni kwa radhi za Allah (SWT). Aidha alieleza kuwa Spirit of Hussein kwa kushirikiana na AFED wamejenga visima kadhaa vya maji katika maeneo kadhaa ya Tanzania ikiwemo katika kituo hiki cha Imam Hussein. Hakika, Kituo hiki kilikuwa ndoto ya Marhum Syed Hassan Naqvi ambaye alikuwa ametembelea Mwanza mwaka wa 2019. Cha kusikitisha ni kwamba mnamo Februari 2021, alirudi kwa Mola wake kabla ya ndoto hiyo kutimia.

      

Alitoa shukrani zake kwa washiriki wa Spirit of Hussein hasa Ndugu. Mohamedraza Badami ambaye aliiwakilisha familia ya Marhum Masoomali Badami aliyefariki Agosti 2023, wakati mradi ukiendelea. Pamoja na Spirit of Hussein, familia ya Badami imetoa mchango mkubwa katika Kituo hiki. Alitamka kwamba Spirit of Hussein ilipewa heshima na bahati ya kukabidhi Kituo hiki kwa Bilal Muslim Mission of Tanzania ikiwa ni kumbukumbu ya Marhum Masoomali Badami na Marhum Syed Hassan Naqvi. Pia alitoa shukurani zake za dhati kwa uongozi wa AFED kwa kujitolea kwao, msaada wao na uchapakazi wao; na akawaombea kwa Allah (SWT) awajaalie tawfeeq zaidi ya kuendelea na kazi tukufu wanayoifanya katika Tabligh, Elimu na Huduma za Kijamii.

Syed Muhammad Naqvi alielezea nia ya Spirit of Hussein kwa kushirikiana na AFED na Bilal Muslim Mission of Tanzania, kujenga kliniki ya uzazi na ina mpango wa kupata ardhi jirani kwa ajili hiyo. Pia alitangaza kwamba Spirit of Hussein itafadhili Iftar kwa siku 30 za mwezi wa Ramadhan katika Kituo hicho kwa miaka 5 na Nyaz kwa siku 10 za Muharram kwa miaka 5.

Syed Ali Raza Naqvi alitoa hotuba ya kusisimua na ya kutia moyo. Kuelekea mwisho, alisisitiza juu ya kile kilichosemwa hapo awali na wazungumzaji na kushukuru juhudi za Bilal Muslim Mission of Tanzania, AFED na Spirit of Hussein kwa maendeleo haya makubwa ya ujenzi wa kituo kwa ajili ya jamii kumwabudu Mwenyezi Mungu (SWT), na pia kitaimarisha umoja na ushirika miongoni mwa jamii zinazoishi karibu na Kituo, ambapo pia kitakuwa na Shule ya Awali.

Kituo hicho kilizinduliwa rasmi na Mgeni Rasmi, Syed Muhammad Naqvi. Aliungana na Alhaj Mohamedraza Badami wa Spirit of Hussein, Mwenyekiti wa AFED Alhaj Amine Nassor na Naibu Kadhi Mkuu wa BAKWATA, Sheikh Ally Ngeruko na wengine. Sherehe ilihitimishwa kwa sala ya Maghribain na chakula cha jioni.

Mwongozaji wa hafla, Sheikh Hashim Maulid aliendesha hafla hiyo vizuri sana na alikuwa mwangalifu katika kutunza wakati kulingana na shughuli za hafla husika.

MATUKIO KATIKA PICHA:

       

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *