RIPOTI – BILAL TANZANIA KATIKA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA IMAM HUSEIN (A)- MUHARRAM, 1444 HIJIRIA

 RIPOTI – BILAL TANZANIA KATIKA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA IMAM HUSEIN (A)- MUHARRAM, 1444 HIJIRIA

Wasifu wa Imam Husein (a)

Jina: Husein (a)

Kin’ya: Aba Abdillahi

Jina la heshima: Sayyidu-Shuhada

Jina la baba: Ali (a)

Jina la mama: Fatima (a)

Tarehe aliyozaliwa: 3 Sha’aban, 4 A.H-Madina

Tarehe aliyouwawa: 10 Muharram 61 A.H-Karbala

Majilis za Muharram – 1444 A.H

Ni utamaduni wa taasisi ya BMMT kufanya majilis (vikao) mfululizo katika kuhifadhi kumbukumbu ya kifo cha Imam Husein (a) pamoja na wafuasi wake takriban 72 wakiwemo watu wa familia yake.

Majilis hizi hufanyika kwenye vituo vyote vya Bilal muslim mission kote nchini kuanzia tarehe mosi hadi 10 – 12 Muharram. Kwa mwaka huu majilis hizo zilianza usiku wa July 31, 2022.

Wakati wa Majilis hizi,Masheikh (Muballighina) huandaa darsa mbalimbali ambazo hutolewa kwa mfululizo kufuatia idadi ya siku zote kama ilivyoelezwa hapo juu. Darsa hizi hutoa fursa kwa waumini kumuelewa Imam Husein (a) na kile kilichosababisha auwawe.

Sababu kubwa iliyopelekea sayyidina husein auawe, ni kupinga dhulma na maovu ya  watawala wa zama hizo wakiongozwa na yazid bin muawiya. Kauli mbiu yake inabainisha wazi kuwa yeye hakupenda udhalimu na maovu mengine ambayo katika kipindi hicho yalikithiri mno ndani ya jamii ya Kiislamu pale aliposema: “Kwa hakika mimi sikutoka kwa sababu ya ujeuri wala majivuno wala kufanya ufisadi wala dhulma. Bila shaka nimetoka kwa ajili ya kuurekebisha umma wa Babu yangu. Nataka niamrishe mema na nikataze maovu….”

Matembezi ya Amani – siku ya Ashura

Kila mwaka inapofika tarehe 10 Muharram, siku ya Ashura, ambayo ndiyo siku aliyouliwa Imam Husein (a), Waislamu wa madhehebu ya Shia Ithnaashari hufanya matembezi ya amani kuitikia wito wa imam Husein (a) aliyoutoa muda mchache kabla ya kuuliwa pale alipopaza sauti akasema, “Je!  Yupo mtu wa kutusaidia na atusaidie?”

Vyanzo mbalimbali vinaarifu kuwa kauli hii ya Imam ulikuwa ni wito kwa kila Muislamu na asiyekuwa Muislamu na kila mpenda haki na amani duniani aunge mkono dhamira ya imam katika suala la kuamrisha mema na kukataza maovu.

Katika kuitikia wito huo, taasisi ya bmmt kama kawaida tuliungana na waislamu wengine duniani kote kumuunga mkono imam Husein (a).

Mafunzo kutoka Karbala

Tukio zima la Karbala kwa ujumla wake limetuachia mafunzo kadhaa ikiwemo kujitolea kwa ajili ya wengine.

Na kwa sababu hiyo basi, BMMT wakati wote imekuwa msatari wa mbele kushiriki shughuli mbalimbali za kuhudumia jamii ikiwemo uchimbaji wa visima kama ishara ya kuwakumbuka wafuasi wa imam husein (a) ambao walinyimwa maji kabla ya kuuliwa. Aidha bmmt kwa jina la Imam Husein (a) imekuwa ikishiriki katika suala la uchangiaji damu kwa wenye kuhitaji damu ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka mashahidi ambao famu yao ilimwagwa huko Karbalaa mnamo mwaka wa 61 (a.h).

Kama ilivyofanyika kwenye miaka ya nyuma, baadhi ya vituo vya Bilal kwa kushirikiana na hospitali mbalimbali za wilaya na mikoa, imeshiriki katika zoezi la uchangiaji damu katika kipindi hiki cha mwezi wa Muharram.

Kwa ujumla damu hii imetolewa kuenzi tukio la Karbala na itatumika kwa mtu yeyote mwenye kuhitaji bila kujali tofauti za kidini au medhehebu.  

Baadhi ya vituo vilivyoshiriki katika zoezi la uchangiaji damu ni pamoja na Bilal Mwanza, Bilal Tanga, Bilal kanda ya Pwani na Kusini.

Uchangiaji damu – Pwani & Kusini

Zoezi la uchangiaji damu kwa upande wa kanda ya Pwani na Kusini, limefanyika kwenye vituo viwili tofauti ambavyo ni Newala mkoani Mtwara na Ikwiriri wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.

Newala

Zoezi la uchangiaji damu limefanyika tarehe 9 August, 2022 katika msikiti wa Bilal- Jamatini na kushirikisha waumini wa Bilal Mtwara pamoja na waumini kutoka vituo vingine vitatu vya Mahuta, Kilidu na Mtama.

Takriban unit 28 za damu zilitolewa kwa ajili ya matumizi katika hospitali ya Wilaya ya Newala.

Ikwiriri

Kwa upande wa tawi la Ikwiriri, zoezi la uchangiaji damu lilifanyika tarehe 9 August, 2022 pia katika msikiti wa Ahlulbayt na liliwashirikisha waumini wa Ikwiriri na wengine kutoka vituo vya Kilimani na Chumbi.

Takriban unit 46 za damu zilipatikana kwa ajili ya matumizi ya hospitali ya wilaya ya Rufiji.

Uchangiaji damu – Mwanza

Kwenye tawi la Bilal Mwanza, jumla ya unit 109 za damu zilipatikana katika zoezi hilo ambalo lilifanyika siku mbili tofauti yaani tarehe 8 na 9 August, 2022. Aidha kwa upande wa tawi hili kulifanyika zoezi la upandaji miti tarehe 10 August ambapo jumla ya miche 1000 ya miti ikiwemo 300 ya matunda na 700 ya mbao ilipandwa katika shule ya msingi Bujingwa.

Uchangiaji damuTanga

Kwa upande wa Bilal kanda ya Tanga, wao wamefanya zoezi la kuchangia damu tarehe 7 August, 2022 katika hospitali ya rufaa ya Bombo mjini Tanga.

NENO LA SHUKRANI

Uongozi wa Bilal Muslim Mission of Tanzania inatoa pongezi kwa wenyeviti wa kanda zote, viongozi, masheikh na waumini wao kwa kuliweka hai tukio la Karbala. Pia inatoa shukrani kwa wahisani wote kutokana na mchango wao wa hali na mali uliosadia ufanikishaji wa matukio haya muhimu.

Mwenyezi Mungu atawalipa zaidi, In sha Allah!

“KILA SIKU NI ASHURA NAKILA ARDHI NI KARBALA”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *