Katika kuendelea kuenzi kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussein (A.S.) na kufikisha ujumbe wa mapambano yake ya Karbala kwa vitendo, vituo vya Bilal Muslim Mission of Tanzania vya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa vimeendesha shughuli mbalimbali za kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya mwezi mtukufu wa Muharram.
Shughuli hizo zimejumuisha zoezi la uchangiaji damu, kutembelea wagonjwa katika vituo vya afya pamoja na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya kijamii. Hatua hizi zimefanyika kwa lengo la kuhuisha mafunzo na misingi aliyosimamia Imam Hussein (A.S.), ikiwemo huruma, kujitolea, kusaidia wenye mahitaji na kuwajibika kwa jamii.
Picha: Baadhi ya waumini baada ya kukamilisha zoezi la uchangiaji damu -Kilimanjaro Siha
Washiriki wa shughuli hizo walipata fursa ya kutoa mchango wao wa damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wahitaji, kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitalini pamoja na kushiriki katika kampeni za usafi zinazolenga kuboresha mazingira ya jamii inayowazunguka.
Wakizungumzia umuhimu wa shughuli hizo, viongozi wa vituo husika walieleza kuwa Muharram si kipindi cha maombolezo pekee, bali pia ni wakati wa kutafakari na kutekeleza kwa vitendo maadili yaliyofundishwa na Imam Hussein (A.S.) katika safari yake ya Karbala, ambapo alisimama kutetea haki, uadilifu na utu wa mwanadamu.
SHEIKH HUSSEIN ZUBEIR – BMMT; akizungumzia uchangiaji wa damu Mwanza .
SHEIKH HASSAN MUHIDIN – BMMT;akizungumzia uchangiaji wa damu kanda ya ziwa
Kwa kutambua juhudi hizo,Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania inaendelea kuhamasisha waumini na jamii kwa ujumla kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii zinazobeba ujumbe wa Karbala, kwa kuzingatia kwamba huduma kwa jamii ni sehemu muhimu ya kuendeleza urithi na mafunzo ya Ahlulbayt (A.S.).
Picha: Waumini Kilimanjaro wakienda kufanya usafi kwenye zahanati
