DAR ES SALAAM, TANZANIA – Makao Makuu ya Taasisi ya Bilal Muslim Mission of Tanzania (BMMT HQ) leo,mei 15,2026 imefanya hafla maalum kwa ajili ya kuwaaga, kuwapa nasaha, na kuwaombea dua maalum mahujaji wanaojiandaa kuelekea Makka kwa ajili ya ibada ya Hijja ya mwaka 2026.
Hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, wadau, na familia za mahujaji, imejawa na mazingira ya kiroho, shukrani, na matumaini makubwa. Mahujaji hawa wamepata fursa hii adhimu kupitia ufadhili mkubwa na wa ukarimu uliotolewa na Bilal Muslim Mission ya Zanzibar.
Katika upande wa mwongozo wa kiroho, Sheikh Hussein Zuberi alisimama kutoa nasaha na za dhati kwa mahujaji hao, akiwakumbusha uzito wa safari wanayoifuata.
Sheikh Hussein alisisitiza kuwa ibada ya Hijja ni ibada muhimu mno ambayo Muumini yeyote aliyebarikiwa kupata fursa hiyo adhimu, anapaswa kubadilika kiakili na kiroho kabla hata hajaondoka.
“Ukipata fursa ya kwenda kuitekeleza ibada hii, jambo la kwanza ni kuepukana na mambo mengine yote ya kidunia. Huu si muda wa biashara, si muda wa mambo yasiyo na tija; ni muda wa kuonyesha uchamungu wa hali ya juu na kuwa mwingi wa ibada kwa ajili ya kuomba rehema za Mwenyezi Mungu,” alisema Sheikh Hussein.
Aliongeza kuwa maeneo matakatifu ni sehemu maalum ya kuchota baraka, kuomba msamaha wa madhambi, na kufanya kila amali itakayomfanya muumini kujikurubisha zaidi na Muumba wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bilal Muslim Mission of Tanzania, Alhaji Hussein Kareem, alisisitiza umuhimu wa kipekee wa ibada hii akisema kuwa inakuja mara moja tu kwa mwaka, hivyo haipaswi kuchezewa.
Alhaji Hussein Kareem aliwasihi mahujaji hao kuhakikisha wanatekeleza ibada hiyo kwa kufuata kikamilifu mienendo na mafundisho ya Ahlul Bayt (a.s), akisisitiza kuwa ndiyo nguzo sahihi inayonyoosha ibada hiyo.
Mbali na ibada yenyewe, Mwenyekiti alitoa wito wa kimkakati akiwataka mahujaji kwenda kuisoma historia ya Uislamu kwa umakini mkubwa wakiwa huko na kueleza kuwa, kihistoria kumekuwa na njama za makusudi kabisa za kufuta na kupoteza ukweli wa historia ya Uislamu, hasa ile inayopitia kwenye mafunzo ya Ahlul Bayt (a.s).
Mwenyekiti wa Bilal Muslim Mission of Tanzania, Alhaji Hussein Kareem
“Nendeni mkaangalie maeneo ya kihistoria kwa jicho la kujifunza. Historia ya Uislamu kupitia mafunzo ya Ahlul Bayt (a.s) imekuwa ikifutwa na kupotezwa kwa makusudi kabisa. Ni wajibu wenu kwenda kujionea ukweli na kuja kuwaelimisha wenzenu,” alisisitiza Alhaji Hussein Kareem.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa Dua Maalum iliyosomwa kwa Pamoja ya kuwaombea mahujaji safari yenye amani, usalama, na afya njema, kwa kibali cha Mwenyezi Mungu ili wapate Hijja Mabrur.
SHEIKH HUSSEIN ZUBEIR