Namakono, Rufiji – Pwani.
Katika kuimarisha juhudi za kujitegemea kiuchumi na kukuza maendeleo endelevu ya jamii, Kituo cha Bilal Muslim Mission of Tanzania kilichopo katika Kijiji cha Namakono, Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani, kimeanzisha mradi wa kilimo cha mkonge kwa ajili ya biashara, kikitumia ardhi inayomilikiwa na kituo hicho.
Mradi huo ni sehemu ya mikakati ya kituo katika kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi, kuongeza fursa za kiuchumi na kujenga msingi imara wa maendeleo ya muda mrefu. Kupitia ushirikiano na mshikamano wa waumini, mradi huu unatarajiwa kuwa chachu ya kukuza uwezo wa kituo kujitegemea na kutekeleza shughuli zake za maendeleo.
Akifafanua falsafa iliyo nyuma ya hatua hiyo, Mwalimu wa Kituo, Sheikh Idrissa Madua, alisisitiza umuhimu wa jamii kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo, alisema:
“Mafanikio ya kijiji huletwa na wanakijiji wenyewe, na mafanikio ya kituo huletwa na wanakituo wenyewe.”
Kauli hiyo inadhihirisha umuhimu wa umiliki wa pamoja, uwajibikaji na matumizi ya nguvu ya jamii katika kujenga maendeleo. Aidha, hatua hii inaonesha namna ambavyo vituo vya Bilal Muslim Mission vinaweza kutumia rasilimali vilizonazo kuanzisha miradi yenye tija na kuimarisha misingi ya kujitegemea.
Bilal Muslim Mission of Tanzania inapongeza uongozi na waumini wote wa Kituo cha Namakono kwa ubunifu, mshikamano na hatua hii ya kuigwa. Ni matumaini ya Taasisi kwamba juhudi hizi zitaendelea kuzaa matunda na kuwa mfano wa kuhamasisha vituo vingine katika kuanzisha miradi ya uzalishaji mali na kujenga uchumi endelevu wa jamii.
Bilal Muslim Mission of Tanzania – Kuelekea Maendeleo Endelevu Kupitia Umoja, Uwajibikaji na Kujitegemea.


