Tarehe 2 Mei, 2024 (23 Shawwal, 1445 Hijiria) Bilal Muslim Mission of Tanzania (BMMT) kwa kushirikiana na Jamiatul Mustafa ilifanya hafla ya usomaji wa Qur’an tukufu, hili lilikuwa moja ya tukio kubwa kufanywa kwa ushirikiano wa taasisi hizo mbili katika mwaka huu, 2024. Tukio hilo lilifanyika Hauzatul Bilal Temeke, Dar es salaam na lilipata heshima ya kuhudhuriwa na Alhaj Aunali Khalfan – Makamu Mwenyekiti wa Africa Federation (AFED). Aidha, tukio hilo lilihudhuriwa na Sheikh Zairai Mkoyogole – Sheikh Mkuu BAKWATA wilaya ya Temeke pamoja na ujumbe wake.
Alhaj Hussein Karim – Mwenyekiti wa BMMT aliambatana na Alhaj Abdul-wahid Mohammed – Makamo Mwenyekiti wa BMMT. Jamiatul Mustafa iliongozwa na Sayyid Arif Ali Naqvi. Wengine waliokuwepo ni Ndugu Hafidhi Mansour – Mtendaji Mkuu BMMT, waalimu wa Hauzatul Bilal Temeke, masheikh kutoka taasisi mbalimbali, wanafunzi na wageni wengine waalikwa kutoka Dar es salaam na maeneo ya jirani.
Hafla hiyo ilifunguliwa kwa kisomo cha Qur’an ikifuatiwa na hotuba ya Alhaj Hussein Karim – Mwenyekiti wa BMMT aliyesisitiza juu ya umuhimu wa kusoma Qur’an lakini pia kuielewa na kutekeleza yale tunayoyasoma badala ya kusoma tu kama wimbo (kusoma bila mazingatio).
Hotuba ya ufunguzi ya mwenyekiti wa BMMT ilifuatiwa na zoezi rasmi la usomaji wa Qur’an. Kwa upande wa Tanzania, Qur’an ilisomwa na Muhammad Haruna, na Muhammad Omar Ndete. Kutoka Iran Qur’an ilisomwa na Yaasin Hassan Gholami na Ghaasim Muqaddami ambao baadae walizawadiwa.
Kabla ya kuhitimishwa kwa hafla hiyo, Alhaj Abdul-wahid Mohammed – Makamo Mwenyekiti wa BMMT alitoa neno la shukran kwa Alhaj Aunali Khalfan kwa niaba ya AFED ambao wametoa mchango mkubwa katika kufanikisha hafla hiyo. Aidha, Alhaj Abdul-wahid Mohammed aliwashukuru wadau wengine wote walioshiriki kufanikisha tukio hilo ikiwa pamoja na wahudhuriaji.
Pembezoni mwa hotuba yake, Alhaj Alhaj Abdul-wahid Mohammed alisisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha umoja na ushirikiano baina ya Waislamu bila kujali itikadi zao za kimadhehebu na kuifanya Qur’an kuwa njia ya utatuzi wa matatizo mbalimbali yanayowakabili waislamu duniani kote.
Mwendeshaji wa hafla hiyo, Samahat Sheikh Msabaha Sha’ban Mapinda ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Tabligh BMMT, aliiongoza vyema hafla hiyo ikiwa pamoja na kuzingatia muda na ratiba ya hafla husika.
MATUKIO KATIKA PICHA: