Kila mwaka uongozi wa Bilal Muslim Mission of Tanzania (BMMT) hukutana na wasimamizi wa kanda pamoja na wakuu wa hawza ili kupokea na kujadili ripoti, kupitia changamoto za kiutendaji, na kubainisha malengo ya mwaka unaofuata. Mikutano hii ni muhimu sana katika kuweka ulinganifu baina ya kanda. Mkutano huo uliwakusisha wasimamizi kutoka Kanda ya Pwani na Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Mkoa wa Kagera, Mkoa ya Tanga, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mkoa wa Tabora, Mkoa wa Kigoma, na Kanda ya Zanzibar. Kila Kanda inasimamia kati ya vituo 10 hadi 65.
Kikao hicho cha siku tatu kilianza Januari 11 – 12, 2024 Hauzat Bilal Temeke na kilihitimishwa Januari 13, 2024 kwenye ukumbi wa mikutano wa Africa Federation (AFED). Hii ni mara ya tatu mfululizo kikao hichi kufanyika.
Mwenyekiti wa BMMT Haj Hussein Karim, Mkamo Mwenyekiti Haj Abdul wahid Mohammed na Mwenyekiti wa BMMT Kanda ya Pwani & Kusini waliongoza vikao hivyo kwa nyakati tofauti tofauti na katika siku ya mwisho, kilipata heshima ya kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa AFED wakiongozwa na Makamo Mwenyekiti wake, Haj Aunali Khalfan pamoja na Mwekahazina – Haj Zainul Chandoo.
Aidha, mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuboeresha Idara ya Tabligh vituoni ilipangwa, hususani katika kunyanyua viwanngo vya taaluma kwenye hauza zetu, ubora wa mafunzo kwenye madrasa zetu, ushiriki wa waumini katika shughuli za uzalishaji mali na uchumi kwa ujumla, ushiriki wa wazazi kwenye safari ya kielimu (dini na akhera) kwa watoto wao.
MATUKIO KATIKA PICHA
KUTOKA AFED:
Alhaj Aunali Khalfan katika hotuba yake aligusia juu ya umuhimu wa kudumisha uhusiano wa kindugu na ndugu zetu wa Kisunni na madhehebu/imani nyinginezo nchini. Aidha, alisisitiza juu ya kujenga mafungamano mapya kwa kutembeleana na kuwaalika katika programu kama vile Maulidi, Iftar za pamoja, Kumbukumbu za matukio ya Karbala n.k.
Alhaj Zainul Chandoo kwa upande wake alizungumzia umuhimu wa utoaji taarifa na ripoti mbalimba kwa wakati, usimamizi thabiti wa fedha za wafadhili, pia alisisitiza haja ya wasimamizi wa Kanda kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa vituo, kufanya ziara za mara kwa mara na kutoa taarifa ili kupata imani ya wafadhili.
Alhaj Hussein Karim aliwashukuru watumishi wa AFED kwa mchango wao kwa BMMT na kuhudhuria kwao katika kikao cha kufunga programu hiyo ya siku 3 kilichomalizika Jumamosi Januari 13 na kupata chakula cha mchana kwa pamoja.
Aidha, BMMT inapenda kutoa shukrani zake kwa AFED kwa kuruhusu matumizi ya kituo chake cha mafunzo kwa ajili ya kufanyika kikao cha mwisho na hafla ya kufunga mkutano huo wa mwaka 2023.
Tunapenda kuwashukuru washiriki wote kutoka Kanda, uongozi wote wa BMMT kwa ushiriki wao na michango yao muhimu katika vikao. Tunatoa shukrani zetu kwa wengine wote ambao kwa namna moja au nyingine walisaidia kufanikisha kikao hiki.
Imetolewa na:
Idara ya Habari na Mahusiano