NAIBU KADHI MKUU WA BAKWATA AFANYA ZIARA BMMT.

  Naibu Kadhi Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) – Alhaj Sheikh Ali Khamis Ngeruko amefanya ziara katika ofisi za Bila Muslim Mission of Tanzania (BMMT) Makao Makuu Dar es Salaam.

Alhaj Sheikh Ngeruko amefanya ziara hiyo mnamo tarehe 10 Januari 2024 akiambatana na ujumbe wake na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa BMMT akiwemo Alhaj Hussein Karim – Mwenyekiti, Alhaj Abdulwahid Mohammed –  Makamo Mwenyekiti, Ndugu Hafidhi Mansour – Mtendaji Mkuu, Samahat Sheikh Msabaha Mapinda – Mkuu wa Idara ya Tabligh, Sheikh Khamis Awadhi – Naibu wa Mkuu wa Idara ya Tabligh na Alhaj AzizHussein Rajani – Mwenyekiti wa BMMT Kanda ya Pwani & Kusini.

Ziara hii ya Naibu Kadhi Mkuu ilikuwa muhimu katika kudumisha mahusiano mema baina ya BAKWATA kama chomo kikuu kinachowaunganisha waislamu hapa nchini na taasisi yetu na ilitoa fursa ya kujadili shughuli mbalimbali zinazofanywa na BMMT na mambo mengine yanayowahusu waislamu wa Tanzania kwa ujumla.

Alhaj Sheikh Ngeruko alivutiwa na historia ya BMMT sambamba na kazi ilizokuwa ikifanya tangu kuasisiwa kwake mnamo mwaka 1968 ikijikita kwenye nyanja ya tabligh, elimu na maendeleo ya kijamii kwa ujumla kama alivyoelezwa na Makamo Mwenyekiti, Alhaj Abdulwahid Mohammed.

Kwa upande wake, Naibu Kadhi Mkuu alitilia mkazo suala la kudumisha umoja baina ya waislamu jambo ambalo limekuwa kipaumbele kwa BAKWATA tangu Mufti na Sheikh Mkuu aliposhika hatamu ya uongozi.

MATUKIO KATIKA PICHA:

   

Picha ya pamoja kutoka kushoto kuelekea kulia: Sheikh Khamis Awadhi, Ndugu Shabani Ally, Alhaj Abdulwahid Mohammed, Alhaj Hussein Karim, Alhaj Sheikh Ali Khamis Ngeruko, Samahat Sheikh Msabaha Mapinda, Ndugu Mudhihir| Picha na: Rajabu Ngwame.

BMMT imefarijika na ziara hii ya Naibu Kadhi Mkuu kwenye ofisi zake na Mwenyekiti, Alhaj Hussein Karim alitilia mkazo umuhimu wa kuendeleza mawasiliano ya marakwamara na anaratajia kuendelea kuona mahusiano chanya baina ya taasisi zetu kwa maslahi mapana ya waislamu wote hapa nchini.

###

Imetolewa na:

Idara ya Habari & Mahusiano

BMMT – Makao Makuu, Dar es Salaam.

About the Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

You may also like these